Michezo

Bora tu Man United wako nyuma yetu EPL, tuna raha duniani, mashabiki wa Arsenal wasema

August 4th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MWENYEKITI wa mashabiki wa timu ya ligi kuu ya Uingereza, Arsenal katika Kaunti ya Murang’a James Nduati anawataka wenzake wazindue awamu za ‘kukaza’ mapema kwa kuwa bado hakuna dalili kuwa msimu huu wa 2019/20 ni wa Arsenal.

Nduati ambaye huongoza ushirikisho wa zaidi ya mashabiki 1, 200 katika Kaunti hiyo ameteta kuwa kocha mpya, Unai Emery hajafanya lolote la kuonyesha kuwa analenga kuinua taji hilo katika utamatisho wa michuano ya msimu huu.

“hata watoto wa chekechea wanajua kuwa shida yetu ndani ya timu ya Arsenal ni ulinzi…Hakuna lolote ambalo Unai Emery amefanya katika soko la kuzimba mianya tele ndani ya ngome yetu…Na kwa wakati mwingine tena, tunakubali utakuwa msimu mgumu kwetu,” akasema.

Hasta hivyo, amesema kuwa kukiri huko sio maana kuwa “tumepoteza matumaini…Hatubanduki kutoka ufuasi wa timu hii yetu tukufu…Timu bora kuiliko Manchester United…Timu yenye ufuasi mkubwa Kenya hii na Afrika kuiliko nyingine yoyote…”

Bw James Nduati, Mwenyekiti wa Mashabiki wa Arsenal kaunti ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Akiwaongoza wafuasi wake, wamesema kuwa asiyekubali kushindwa basi ako na yake mengine nje ya spoti na wakati mambo yanawaendea mrama kufuatia vichapo kimo cha mburukenge , huwa wanakubali matokeo.

“Hujatuona tuukijiapisha au tukipinga matokeo licha ya kuwa Kinara wa Upinzani Nchini Kenya, raila Odinga ni mmoja wetu ndani ya ufuasi wa Arsenal…Bado tuko ngangari hata tuchapwe kwa kuwa hiyo ndiyo hali ya kimchezo na ndani ya Arsenal tunaelewa kuwa tunaweza katika kila mechi tukashindwa, au tushinde au twende droo,” asema Bw Nduati.

Alisema kuwa ligi hiyo ikiwa na timu 20 na kila moja ya hizo zote ikilenga ushindani wa kupata ushindi, Arsenal ikipata leo, ipoteze kesho na tena ipoteze ikitarajia kupata sio hali isiyo ya kawaida.”

Akasema: “Mpira ukidunda na ukukatae, hata ufanye nini huwezi ukajinusuru. Kwa sasa umetukataa na hilo ndilo suala la kukubali. Tuiname na timu na tuinuke na timu. Huo ndio ujumbe wangu mkuu kwa leo.”

Amesema kuwa “kuunga mkono Arsenal kila msimu ingawa ni sawa na ile taswira sawa na kumuunga Mkono Raila Odinga kuwa rais wa Kenya au kuunga mkono timu ya Harambee Stars yetu hapa Kenya kutwaa taji la ulimwengu katika soka,” bado matumaini yako hai.

Lakini amekiri kuwa kwa sasa wafuasi wa Arsenal katika eneo hilo hawana la kutumainia kwa ubabe wa kutwaa taji hata la Europa, “lakini sio kumaanisha sisi tutawapa raha mashabiki wengine hasa wale wa Man United..Lengo letu kuu ni kumaliza juu ya Man United katika jedwali.”

Amesema kuwa hata wakati mambo yamekuwa mabaya zaidi katika , ulingo wa EPL, “bora tu Man United iko nyuma yetu, hata tushushwe daraja tukiwa nambari 19 na Man United iwe nambari 20 katika jedwali, sisi tuko sawa.”