Habari za Kitaifa

Bora uhai: Maazimio ya wengi 2024

January 1st, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

HUKU sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zikizidi kunoga kote nchini, idadi kubwa ya Wakenya hawakuandaa maazimio yoyote ya 2024, Taifa Leo Dijitali imebaini.

Tofauti na miaka mingine ambapo watu hujishughulisha na kuorodhesha maazimio wanayokusudia kutimiza mwaka mpya, 2024 huenda ikawa tofauti huku Wakenya wakiibua hisia mseto.

Kulingana na udadisi uliofanywa jana na Taifa Leo Dijitali, hali mbaya ya kiuchumi ikiwemo bei ghali ya bidhaa za kimsingi, gharama ya juu ya maisha, kuongezeka kwa ada za ushuru ni sababu kuu zilizowakatiza tamaa wananchi.

Bw Omar Ali, mfanyabiashara jijini Nairobi ni miongoni mwa waliojiepusha na kuandaa maazimio yoyote akitumia msemo maarufu ‘bora uhai’.

Mfanyabiashara huyo anasema kufuatia pandashuka alizoshuhudia mwaka uliopita, 2023, cha muhimu kwake sasa ni uzima na afya njema kwake na wapendwa wake.

“Maazimio yapo lakini kuna haja gani ya kuyandaa? Mambo ni magumu sana, kama wazazi tunajishughulisha na tutakapotoa hela za kuwalipia karo watoto wetu, bei za bidhaa za kimsingi ikiwemo vyakula zimepanda, hali si hali. Kilicho muhimu tu sasa ni uhai na afya njema,” anasema.

Hisia zake ni sawia na za Luke Waweru, anayesema kwamba atalazimika kuendelea na maazimio aliyoshindwa kutimiza 2023 kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Japo alianza 2023 kwa matumaini tele, anafichua hakuweza kutimiza malengo yake yote huku akitoa wito kwa Rais William Ruto kuwapunguzia Wakenya mzigo wa ada za ushuru.

Hata hivyo, kuna baadhi waliokwisha andaa maazimio yao huku wakijawa na matumaini kuhusu mwaka huu mpya.

Paul Makau anasema kuwa “Mwaka huu wa 2024 ninaazimia kujitenga kabisa na chochote kisichonufaisha maisha yangu. Iwe ni tabia, kitu au mtu yoyote asiyeongeza thamani katika maisha yangu sitaki kamwe.”

Kupunguza muda wanaotumia kwenye simu, kuwa na subira zaidi, nidhamu na uzingativu ni miongoni mwa maazimio ambayo idadi kubwa ya wazazi wanakusudia kutimiza mwaka huu kwa mujibu wa utafiti mpya.

Kulingana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Michigan, idadi kubwa ya wazazi, zaidi ya asilimia 50, wamepania kupunguza muda wanaotumia kwenye simu huku asilimia 75 wanataka kuwa na subira zaidi.

Ripoti hiyo inaashiria kuwa “matukio makuu kama vile mwanzo wa mwaka au shule hupatia familia motisha wa kuboresha afya yao kimwili na kihisia, ikiwemo kutafakari.

“Katika juhudi za kuboresha malezi yao, wazazi hutilia maanani zaidi jinsi wanavyoweza kuboresha afya yao na ya watoto wao, kuimarisha ushikamano wa watoto wao na jamii kwa jumla na kuhusika zaidi kwenye maisha ya wapendwa wao.”

Kuhusu afya na mazoezi, karibu nusu ya wazazi waliohojiwa wamepania kuwapa wapendwa wao vyakula na vitafunio vyenye manufaa kiafya huku wengine wakipanga kuwashirikisha watoto wao kufanya mazoezi pamoja.