BORESHA AFYA: Kukabili uvundo kinywani

BORESHA AFYA: Kukabili uvundo kinywani

NA PAULINE ONGAJI

TATIZO la kutoa harufu mbaya kinywani hutokana na mambo mengi.

Lakini je wajua kuna vyakula kukusaidia kukabiliana na shida hii? Kwa mfano:

•Maji: Unapokunywa maji, unasuuza chembechembe za masalio ya chakula na seli zilizokufa, na hivyo kuzuia bakteria zinazosababisha harufu mbaya kuzaana kinywani mwako.

•Mboga na matunda: Mboga na matunda kama vile tufaha, karoti na pea husaidia kuzalisha mate mdomoni ambayo husaidia kusafisha bakteria zinazosababisha harufu mbaya kinywani.

•Tikiti maji na matunda jamii ya machungwa: Matunda haya yana viwango vya juu vya vitamini C ambayo husaidia kusafisha kinywa na kuzuia bakteria zinazosababisha maradhi na matatizo mengine ya kinywani kama vile halitosis na gingivitis. Aidha cheri husaidia kuondoa harufu ya gesi ya methyl mercaptan, ambayo hupatikana katika vyakula kama vile vitunguu na chizi, na ambayo husababisha harufu mbaya kinywani.

•Tangawizi: Ina kiungo kinachoitwa 6-gingerol, kinachochochea kimeng’enyo kwenye mate ambacho husaidia kuvunjavunja madini ya sulphur kinywani. Jaribu kuchanganya tangawizi, juisi ya ndimu na maji moto kusuuza mdomo.•Chai ya kijani: Tafiti zinaonyesha kwamba viungo vilivyo kwenye kinywaji hiki husaidia kukabiliana na bakteria zinazosababisha harufu mbaya kinywani.

•Chingamu isiyo na sukari: Husaidia kuyeyusha na kuondoa chembechembe za masalio ya chakula na seli zilizokufa kwenye meno, ambazo husababisha harufu mbaya kinywani.

• ‘Chlorophyll’: Kiungo hiki kinapatikana kwenye mboga za kijani au kama kijalizo na husaidia kupunguza harufu mbaya kinywani.

• ‘Yoghurt’ iliyo na probiotics: Aina hii ya mtindi huwa na bakteria nzuri na yaweza kusaidia kukabiliana na bakteria zinazosababisha harufu mbaya mdomoni.

  • Tags

You can share this post!

Manufaa ya poda ya fenugriki

Man-City wasajili beki Sergio Gomez kujaza pengo la...

T L