Borussia Dortmund waajiri kocha Edin Terzic

Borussia Dortmund waajiri kocha Edin Terzic

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund wamemteua Edin Terzic kuwa mkufunzi wao mpya kwa mkataba wa miaka mitatu hadi 2025.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 39 anajaza pengo la Marco Rose aliyetimuliwa mnamo Mei 2022 baada ya msimu mmoja pekee kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Terzic ambaye ni raia wa Ujerumani, aliwahi kudhibiti mikoba ya Dortmund kwa muda mfupi akiwa kocha mshikilizi mnamo 2020-21 kabla ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa benchi ya kiufundi.

“Edin anaifahamu klabu hii vizuri na falsafa ya kikosi chetu. Tutategemea pakubwa tajriba yake ya ukufunzi kutwaa mataji kadhaa msimu ujao wa 2022-23,” akasema mkurugenzi wa soka kambini mwa Dortmund, Sebastian Kehl.

Terzic alianza ukocha akidhibiti mikoba ya chipukizi wa Dortmund kati ya 2010 na 2013 kabla ya kuaminiwa fursa ya kuwa msaidizi wa Slaven Bilic kambini mwa Besiktas ya Ligi Kuu ya Uturuki.

Alimfuata Bilic kambini mwa West Ham United katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2015 kabla ya kuondoka baada ya mkufunzi huyo raia wa Croatia kutimuliwa mnamo Novemba 2017.

Alirejea kambini mwa Dortmund kuwa msaidizi wa Lucien Favre mwanzoni mwa 2018 na akateuliwa kushikilia mikoba ya kikosi hicho baada ya Favre kupigwa kalamu mnamo Disemba 2020. Aliongoza kikosi chake hicho kutwaa taji la German Cup mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mourinho aongoza AS Roma kutandika Feyenoord na kutwaa taji...

Utengano kati ya Uhuru na Ruto wadhihirika hata katika...

T L