Borussia Dortmund waendeleza ufufuo wao kwenye Bundesliga na kufuzu kwa soka ya UEFA msimu ujao

Borussia Dortmund waendeleza ufufuo wao kwenye Bundesliga na kufuzu kwa soka ya UEFA msimu ujao

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund walifuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya 10 katika kipindi cha misimu 11 baada ya kuwacharaza Mainz 3-1 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumapili.

Ufanisi huo huenda ukaimarisha zaidi nafasi yao ya kuwadumisha kikosi wanasoka tegemeo kama vile Erling Braut Haaland na Jadon Sancho wanaowaniwa pakubwa na vikosi maarufu vya bara Ulaya.

Kufikia mwanzo wa Aprili 2021, pengo la alama saba lilikuwa likiwatenganisha Dortmund na kikosi cha Bayer Leverkusen kilichokuwa kikishikilia nafasi ya nne jedwalini. Hata hivyo, Dortmund walijikakamua vilivyo na kusajili ushindi katika jumla ya michuano sita za ligi tangu wakati huo – matokeo yaliyoshuhudia Leverkusen wakishuka hadi nafasi ya sita kwa alama 52, tano nyuma ya nambari tano Eintracht Frankfurt.

Kufikia sasa, Dortmund wanajivunia pointi 61 sawa na nambari nne VfL Wolfsburg na ni pengo la alama nne ndilo linatamalaki kati yao na RB Leipzig watakaokamilisha kampeni za Bundesliga msimu huu katika nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich ambao tayari wamefaulu kuhifadhi ufalme wa kipute hicho.

Mabao ya Dortmund dhidi ya Mainz mnamo Jumapili yalifumwa wavuni kupitia wanasoka Raphael Guerreiro, Marco Reus na Julian Brandt. Mainz walifutiwa machozi na Robin Quaison kupitia penalti ya dakika za mwisho wa kipindi cha pili.

Dortmund walishuka dimbani kwa ajili ya mchuano huo wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakiwachabanga Leipzig 4-1 mnamo Mei 13 na kutia kapuni ubingwa wa German Cup.

“Si watu wengi walituamini. Lakini tulisalia imara na hatukutetereka. Kila mtu alijituma kikosini na bidii zao zimezaa matunda yanayoonekana. Tuna ulazima wa kujituna zaidi na tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa uwanjani,” akasema nahodha wa Dortmund, Marco Reus.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kipa Alisson Becker awapa Liverpool tumaini la kukamilisha...

Mshindi wa Ligue 1 msimu huu kujulikana siku ya mwisho ya...