Borussia Monchengladbach watoka nyuma na kuzamisha chombo cha Bayern Munich ligini

Borussia Monchengladbach watoka nyuma na kuzamisha chombo cha Bayern Munich ligini

Na MASHIRIKA

VIONGOZI wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich walipoteza uongozi wao wa 2-0 dhidi ya Borussia Monchengladbach na kuambulia kichapo cha 3-2 mnamo Januari 8, 2021.

Hiyo ilikuwa mara ya nne kwa Bayern kupoteza mechi chini ya kocha Hansi Flick ambaye kwa sasa wamewaongoza katika jumla ya michuano 60.

Bayern walichukua uongozi kupitia penalti ya fowadi Robert Lewandowski katika dakika ya 20 kabla ya Leon Goretzka kuvurumisha kombora kutoka hatua ya 20 na kutikisa nyavu za wenyeji wao katika dakika ya 26.

Hata hivyo, Jonas Hofman aliwarejesha M’gladbach mchezoni kwa kufunga mabao mawili katika dakika za 35 na 45 baada ya kukamilisha krosi za Lars Stindl kwa ustadi mkubwa.

Florian Neuhaus alipachika wavuni bao la tatu kwa upande M’gladbach katika dakika ya 49 na kuongoza waajiri wake kupaa hadi nafasi ya saba jedwalini kwa alama 24 sawa na Union Berlin na VfL Wolfsburg.

Mechi mbili ambazo kocha Hansi alishuhudia Bayern wakipoteza akidhibiti mikoba ya miamba hao wa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika msimu wa 2019-20 zilikuwa dhidi ya M’gladbach.

Licha ya kichapo, Bayern bado wanaselelea kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 33, mbili mbele ya nambari mbili RB Leipzig ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimesakatwa na Bayern.

You can share this post!

RIZIKI: Ushonaji nguo unahitaji utafiti wa kutosha kuelewa...

Kenya Morans kuingia kambini Januari 11 kwa mechi za kufuzu...