Shangazi Akujibu

Bosi humenya tunda la mfanyakazi mwenzangu; sijui kwa nini bado ananifuata

July 3rd, 2024 1 min read

Shangazi,

Bosi wangu ananitaka kimapenzi na ameahidi kunipa chochote ninachotaka. Ninajua anataka kunitumia tu kwa sababu ana uhusiano na mwanamke mwingine tunayefanya kazi pamoja. Naogopa kwamba nikikataa nitafutwa kazi. Nifanyeje?

Ni muhimu kuheshimu nafsi yako. Mwambie bosi wako wazi kwamba huwezi kuwa na uhusiano naye kwa sababu unajua ana mpenzi. Ni heri akufute kazi lakini udumishe heshima yako.

Mapenzi yameanza kuathiri masomo yangu

Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili. Nimependana na kijana jirani yetu mtaani. Mapenzi yetu yameanza kuathiri vibaya masomo yangu na nataka kumuacha. Nimemwambia lakini amekataa. Nifanye nini?

Mapenzi ni sumu kwa mwanafunzi kama wewe. Ni vizuri umegundua kwamba ulifanya makosa. Uliingia katika uhusiano huo kwa kupenda na kama hutaki kuendelea huwezi kulazimishwa.

Ninampenda mwanamke anayenizidi kwa miaka 10

Mpenzi wangu alikuwa ameolewa lakini akakosana na mumewe na kuondoka na mtoto wao. Nataka kumuoa lakini najua wazazi wangu watashangaa kwa sababu amenizidi umri kwa karibu miaka kumi. Nishauri.

Usijali watu watasema nini kuhusu mwelekeo unaochukua maishani bora tu unaamini ndio unaofaa. Kama umempenda mwanamke huyo na unahisi ndiye anayefaa kuwa mke wako usiogope kusemwa.

Wakwe hawanitaki licha ya kuwa kwenye ndoa miaka miwili, ushauri?

Nimekuwa katika ndoa kwa miaka miwili. Wazazi wa mume wangu wamepinga ndoa yetu na wameniambia hawanitaki. Isitoshe, mume wangu bado hajaenda kwetu. Nampenda lakini mambo hayo yananitatiza.

Ni makosa kwamba mume wako hajaona maana ya kwenda kwenu kujitambulisha kwa wazazi miaka miwili ambayo mmeishi pamoja. Pili, wazazi wake hawakutambui wewe wala wazazi wako. Nahisi unapigania ndoa isiyo na matumaini.