Habari Mseto

Boti mpya la kushughulikia mikasa baharini lazinduliwa

June 25th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

Kaunti ya Lamu imezindua boti maalum litakaloshughulikia kuokoa wasafiri wakati ajali za boti na mashua zinapotokea baharini.

Boti hiyo kwa jina MV Bajuni, lilizinduliwa kwenye sherehe ya kufana iliyoongozwa na Gavana wa Lamu, Fahim Twaha Jumapili katika kisiwa cha Lamu.

Kwa muda mrefu wakazi wa Lamu wamekuwa wakilalamikia kukosekana kwa miundombinu ya kushughulikia mikasa ya baharini kila inapotokea eneo hilo, jambo ambalo kila wakati hupelekea maisha ya wakazi kuangamia baharini.

Boti hilo lilinunuliwa chini ya udhamini mkuu wa Wakfu wa Jaffer (Jafar Foundation).

Gavana wa Lamu Fahim Twaha akizindua rasmi boti la kuokoa wakazi wakati wa mikasa ya baharini. Boti hiypo ilinunuliwa chini ya udhamini wa wakfu wa Jaffer. Picha/ Kalume Kazungu

Akihutubia umma wakati wa uzinduzi wa boti hiyo, Gavana Twaha alisema kaunti itajitolea kwa dhati ili kuzuia maafa baharini wakati ajali za boti zinapotokea.

Alishukuru wakfu wa Jaffer kwa kujitolea kwake kusaidia kaunti ya Lamu kwa boti hiyo.

“Tunashukuru kwamba leo tunazindua rasmi boti la kuokoa maisha ya wakazi hasa majanga ya baharini yanapotokea. Boti hili litakuwa likishika doria kwenye Bahari Hindi eneo la Lamu na kuhakikisha inasaidia shughuli za uokoaji punde ajali zinapotokea. Tutaendelea kushirikiana na wahisani mbalimbali ili kuhakikisha maisha ya wakazi yanakingwa baharini,” akasema Bw Twaha.

Bw Twaha na afisa wa wakfu wa Jaffer Foundation, Mohamed Jaffer, akikabidhiwa funguo za boti hilo. Picha/ Kalume Kazungu

Alisema kaunti pia ina pmango wa kununua maboti zaidi yatakayosaidia kuokoa wakazi punde ajali za boti zitokeapo baharini.

Naye Afisa Mkuu wa Wakfu wa Jaffer, Bw Mohamed Jaffer, alisema lengo lao ni kusaidia kaunti kuafikia maendeleo.

Alisema mbali na boti, pia wakfu wake utatoa Sh 1 milioni kusaidia vikundi vya akina mama eneo hilo.

Alisema pia atashirikiana na serikali ya kaunti ya Lamu ili kununua boti zaidi zitakazosaidia kusafirisha wagonjwa hospitalini hasa kutoka maeneo ya visiwani.

Kazi ya kushughulikia mikasa baharini yaanza. Picha/ Kalume Kazungu

“Tumetoa boti hii lakini haitoshi. Tuna mpango wa kutoa ambulensi ya baharini ambayo itashughulikia kubeba wagonjwa visiwani na kuwapeleka mahospitalini. Pia tutasaidiana na kaunti ili kuinua vikundi vya akina mama, vijana na walemavu eneo hili,” akasema Bw Jaffer.

Mnamo Machi mwaka huu, serikali ya kaunti ya Lamu ilipokea msaada wa boti ya kima cha Sh 10.5 million ambayo ni ya kusaidia kubeba wagonjwa kutoka maeneo ya visiwani kuwafikisha kwenye hospitali mbalimbali za Lamu.

Boti hiyo ilinunuliwa na Shirika la USAID Afya Pwani.