Michezo

Bournemouth ilivyotikiswa na Covid-19

June 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

HABARI za kipa Aaron Ramsdale kupatikana na virusi vya ugonjwa wa Covid-19 zilitikisa pakubwa kikosi kizima cha Bournemouth.

Haya ni kwa mujibu wa kocha wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Eddie Howe.

Ramsdale, 22, ambaye hakuwa na dalili zozote za kuwa na virusi vya corona ni miongoni mwa watu wanane ambao kwa sasa wanaugua Covid-19 miongoni mwa wachezaji na maafisa wa klabu zote 20 za EPL.

“Wazia hofu ilivyowavaa wanasoka wengine kikosini. Fikiria kuhusu unyanyapaa na uoga ambao kwa sasa kikosi kizima kinapitia baada ya kutangamana kwa karibu na Ramsdale,” akatanguliza Howe.

“Kabla ya kisa chochote kuripotiwa miongoni mwa wachezaji na maafisa kikosini, sote tulikuwa tukijihisi sawa. Maisha yalikuwa sawa, udugu ulikita mizizi na kila kitu kilikuwa kawaida. Lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa na saikolojia ya wachezaji na hata wakufunzi imeathirika sana,” akasema mkufunzi huyo mzawa wa Uingereza.

“Hata tunaposubiri matokeo ya vipimo vijavyo, sote kwa sasa ni roho mkononi. Hakuna anayelala unono kila mara anapowazia kuhusu uwezekano wa kupatikana na virusi vya corona kisha kutupwa karantini kwa siku saba.”

Hadi kufikia sasa, ni visa tisa vya maambukizi ya corona vimeripotiwa katika vikosi vya EPL baada ya zaidi ya watu 2,000 wakiwemo vibarua, wafanyakazi, wachezaji, makocha, marefa na maafisa wa klabu mbalimbali kufanyiwa vipimo vya afya. Mbali na Ramsdale, miongoni mwa waliopatikana na virusi vya corona hivi karibuni zaidi ni beki Adrian Mariappa wa Watford na kocha msaidizi wa Burnley, Ian Woan.

Matokeo ya raundi ya nne ya vipimo vya Covid-19 yanatarajiwa kutolewa baadaye Jumatano ya Juni 3, 2020.

Vikosi vya EPL vilianza mazoezi katika vikundi vya watu watano mnamo Mei 19 kwa mara ya kwanza tangu kipute hicho kiahirishwe mnamo Machi 13 huku zikiwa zimesalia mechi 92 katika kampeni za msimu huu.

Baada ya klabu kupiga kura itakayoshuhudia wanasoka wakirejelea mazoezi ya kawaida kambini mwao, vinara wa vikosi vyote 20 vinatarajiwa kuandaa kikao kingine Alhamisi ya Juni 4 kutafuta mwafaka kuhusiana na viwanja vitakavyotumiwa.

Mengine yatakayojadiliwa ni jinsi ya kurejesha fedha za waliokuwa wapeperushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya mechi za EPL na namna ambavyo kampeni za muhula huu zitatamatishwa iwapo ligi hiyo italazimika tena kusitishwa pindi baada ya kurejelewa.

Bournemouth, Watford, Brighton na Aston Villa ni miongoni mwa klabu ambazo zimepinga mipango ya kurejelewa haraka kwa kivumbi cha EPL kabla ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo.