Michezo

Bournemouth kuchuana na Man-City kwenye Carabao Cup

September 17th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BOURNEMOUTH waliwapiga Crystal Palace 11-10 kupitia mikwaju ya penalti kwenye raundi ya pili ya Carabao Cup baada ya kuambulia sare tasa mwishoni mwa dakika 90 mnamo Septemba 15, 2020.

Ushindi wa Bournemouth uliwakatia tiketi ya kuchuana sasa na mabingwa watetezi Manchester City kwenye raundi ya tatu wiki ijayo.

Baada ya wanasoka wote 20 (isipokuwa makipa), kufunga penalti zao, mlinda-lango Wayne Hennessey aliudaka mkwaju wa kipa Asmir Begovic wa Bournemouth kabla yay eye mwenyewe kuupaisha mkwaju wake juu ya mlingoti.

David Brooks alifunga mkwaju wake wa pili wakati wa kuchanjwa kwa penalti huku Begovic akipangua kombora la Luka Milivojevic kwa upande wa Bournemouth na kuwapa fursa ya kusonga mbele.

Bournemouth walitamalaki mchezo, wakawazidi maarifa wapinzani wao katika takriban kila idara na kuwaelekezea makombora 17 yaliyolenga shabaha. Palace walifanya majaribio manne pekee langoni pa Bournemouth walioshushwa daraja kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu wa 2019-20 baada ya kipindi cha miaka mitano.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO