Makala

BRACHIARIA: Siri ya kupunguza gharama ya kuzalisha maziwa

September 24th, 2020 4 min read

Na DAVID MUCHUI

MFUGAJI Kenneth Kimathi, huwafuga ng’ombe wa maziwa huko Ntharene, Imenti Kusini, Kaunti ya Meru.

Anatukaribisha nyumbani kwake mita chache kutoka barabara kuu ya Meru-Embu karibu na soko maarufu la ndizi.

Tunapowasili, wafanyikazi wanajishughulisha kupanua banda lake la ng’ombe wa maziwa huku mwingine akitayarisha mzigo wa nyasi ya Nandi Setaria kwa chakula cha ng’ombe cha siku hiyo.

Tunakaa chini ya kivuli huku Bwana Kimathi akisimulia safari yake ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na jinsi alivyofanikiwa kupunguza gharama ya uzalishaji wa maziwa kwa asilimia hamsini.

Kulingana na mkulima huyu maarufu, siri iko katika shamba la ekari moja karibu mita 200 kutoka nyumbani kwake ambapo hupanda nyasi aina ya Brachiaria. Nyasi hii inapigiwa upatu kama suluhu ya shida ya lishe kwa wafugaji wa maziwa.

Bw Kimathi, ambaye ni mwalimu aliyestaafu mapema ili kuzingatia kilimo, anasema mafanikio yake yanatokana na kusoma kutokana na wakulima waliofaulu.

Baada ya kutembelea wakulima wengine, aligundua nyasi aina ya Brachiaria, ambayo wanasayansi wanasema ina uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa maziwa na pia afya ya mifugo.

“Nilijitosa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa mnamo 2010. Nilianza ufugaji na ng’ombe watatu ambao wameongezeka hadi ishirini. Hadi 2018, nilikuwa nikitumia zaidi ya Sh70, 000 kwenye chakula cha ng’ombe kwa mwezi. Leo, ninatumia karibu Sh45, 000 kwa malisho kwa ng’ombe wote ishirini.”

“Kwa kutumia brachiaria, nilipunguza gharama ya kuzalisha lita moja ya maziwa hadi Sh15 na wakati huo huo kuongeza uzalishaji kwa kila ng’ombe,” Bw Kimathi anasema.

Anasema ufugaji wake ulibadilika mwaka wa 2017 baada ya kutembelea shamba moja kule Tala, Machakos ambapo mkulima aliwajulisha brachiaria.

Kwa msaada kutoka kwa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo la Kenya (Kalro), Kimathi alipata mifuko miwili ya mbegu ya brachiaria aina ya Mulato 2.

Baadaye mnamo 2018, alipata aina bora ya mbegu zinazotengenezwa na Kalro, kama vile Piata, Xaraes, MG4 na Basilisk. Mbegu hizi zinafanyiwa utafiti na Kalro na bado hazijaanza kuuzwa.

“Baada ya kulinganisha sifa za mbegu hizi, nilichagua Piata na Xaraes ambazo zina uzito na uzani zaidi,” Kimathi anaelezea.

Anasema kuwa brachiaria aina ya Mulato 2 hupunguza uzalishaji baada ya miaka mitatu ilhali Piata na Xaraes hutoa lishe zaidi kwa kila mche.

INUKA

Mkulima huyo anasema biashara yake ya maziwa iliinuka wakati alianza kulisha ng’ombe wake na nyasi ya brachiaria.

“Brachiaria ilisaidia kukata kiwango cha chakula kwa ng’ombe kwa kiasi kikubwa na wakati huo huo uzalishaji wa maziwa uliongezeka. Wakati wa uzalishaji uko kileleni, ninapata zaidi ya lita mia mbili. Ng’ombe pia zikawa na afya,” anasema.

Kulingana na Bw Murithi, Brachiaria, huwa na protini ghafi ya hadi asilimia 20 na ukavu wa unaokaribia asilimia 80, viwango ambavyo ni muhimu kwa utzalishaji wa maziwa.

“Ng’ombe wa maziwa anahitaji protini ghafi ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa. Lishe inapaswa pia kuwa na ukavu mwingi ili ng’ombe anywe maji ya kutosha kutengeneza maziwa. Brachiaria ina sifa hizi zote mbili hivyo kuifanya nyasi ya ajabu kwa ng’ombe wa maziwa,” Bw Kimathi anaelezea.

Aidha, brachiaria hukua haraka baada ya kuvuna, hutoa majani zaidi kwa muda mfupi, huvumilia ukame na inaweza kuvunwa kwa miaka 10 mtawalia.

Brachiaria inaweza kulishwa ikiwa mbichi au kuhifadhiwa kwa ikiwa kavu.

Bw Kimathi ana maghala mawili ambayo anahifadhi takriban tani 16 za nyasi ya ng’ombe.

Ili kuifanya brachiaria iweze kupendeza zaidi, Kimathi huikata kwa mashine na kuchanganya kilo kumi za brachiaria na kilo mbili za ngano na kilo mbili za maize jam kwa kila ng’ombe kwa siku.

“Pia ninaongeza dawa ya kupungiza aflatoxin, molasses na nyasi za kijani za Nandi Setaria kwenye malisho. Mchanganyiko huu unanipa asilimia 24 ya protini ghafi ambayo ni ngumu kupata katika chakula cha dukani,” anasema.

Kabla ya kuanza kutumia brachiaria, Kimathi anasema gharama yake ya uzalishaji ilikuwa zaidi ya Sh30 kwa lita kwani ilibidi anunue mabua ya mahindi, nyasi, nyasi ya Napier na unga.

“Wakati wa kiangazi, nilitumia wakati na pesa nyingi kutafuta nyasi kule Tharaka, Mwea na Timau. Hii ilifanya gharama za uzalishaji wa maziwa kuwa juu sana,” anasimulia.

Hivi sasa, mkulima huyu anauza karibu lita 90 za maziwa kwa Meru Central Dairy Cooperative Union ambao hununua lita moja kwa Sh32 akipata faida ya Sh1, 530 kila siku.

Wakati shule zimefunguliwa, faida yake hupanda kwani anauza lita 30 za maziwa katika shule jirani kwa Sh50 kwa lita.

Mbali na kulisha mifugo, Bw Kimathi huuza miche ya Brachiaria kwa Sh1000 kwa mfuko wa kilo hamsini.

Pia anatarajia kuanza ufugaji (baling) wa nyasi ya brachiaria kwa kuuza kwa wakulima.

Ili kukidhi mahitaji ya mifugo yake na wakulima wengine, Kimathi amepanda nyasi katika ekari nyingine mbili na nusu.

Kulingana na Dkt Donald Njarui ambaye ni mwanasayansi anayehusika na ukuzaji Brachiaria katika Kalro, nyasi hii sio nzuri tu kwa lishe lakini pia inasaidia katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Anasema ikilinganishwa na nyasi ya Napier, brachiaria haina gharama kubwa kuisimamia na inasagwa vizuri na tumbo la ng’ombe hivyo kupunguza uzalishaji wa methane.

Dkt Njarui anasema nyasi hiyo bado haijaanza kuuzwa kwani inathibitishwa na Huduma ya Ukaguzi wa Afya ya mimea ya Kenya (Kephis).

“Tumekuwa tukipeana mbegu kwa wakulima bila malipo ili kufanya majaribio. Majaribio haya yametuwezesha kuchagua aina nne bora za brachiaria. Ripoti kutoka kwa wakulima zinaonyesha kuwa brachiaria inapunguza utumiaji wa chakula cha ng’ombe hadi asilimia 50,” Dkt Njarui anasema.

Mbali na hayo, anasema brachiaria ina uwezo wa kuongeza uzalishaji wa maziwa huku ikiimarisha ubora wa maziwa.

“Tunapendekeza kwamba wakati wa kupanda mbegu, safu hizo zitengane kwa sentimita 50. Mkulima anahitaji kilo tano hadi saba za mbegu kwa hekta moja. Nafasi kati ya mimea inastahili kuwa sentimita 30,” Dkt Njarui anashauri.

Anapendekeza matumizi ya mbolea yawe tani tano hadi 12 kwa hekta. Mkulima anaweza pia kutumia triple superphosphate au samadi ya CAN wakati wa kupanda.

Brachiaria inaweza kutoa hadi tani 20 za lishe ya kijani kwa ekari moja na huvunwa miezi minne baada ya kupanda na kukatwa kila baada ya miezi miwili kwa miaka 10.