Brazil wala njama ya kufinya Korea Kusini

Brazil wala njama ya kufinya Korea Kusini

NA MASHIRIKA

BRAZIL watashuka leo Jumatatu uwanjani 974 nchini Qatar kwa kibarua kizito cha kudengua Korea Kusini katika raundi ya 16-bora na kuweka hai matumaini ya kunyanyua Kombe la Dunia kwa mara ya sita.

Mshindi wa gozi hilo atamenyana na kikosi na mshindi mwingine wa duru hiyo baina ya Japan na wanafainali wa Kombe la Dunia 2018, Croatia, ugani Al Janoub.

Chini ya kocha Adenor Bacchi ‘Tite’, Brazil waliwapiga kumbo Uswisi kwa wingi wa mabao na kutawala Kundi G kwa alama sita, mbili mbele ya Cameroon na tano zaidi kuliko Serbia.

Wafalme hao mara tano wa dunia (1958, 1962, 1970, 1994, 2002) walianza kampeni za Kundi G kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Serbia kabla ya kulaza Uswisi 1-0 kisha kucharazwa 1-0 na Cameroon katika mechi iliyoshuhudia Tite akifanyia kikosi chake mabadiliko 10.

Kichapo hicho kutoka kwa Cameroon kilikomesha rekodi nzuri ya kutopigwa kwa Brazil katika michuano tisa mfululizo.

Hata hivyo, miamba hao bado wanapigiwa upatu kutwaa ubingwa wa mwaka huu licha ya kutofunga bao katika kipindi cha kwanza kwenye mapambano matano yaliyopita ya Kombe la Dunia.

Brazil wamefuzu kwa raundi za muondoano kwenye Kombe la Dunia mara tisa mfululizo na miaka 32 imepita tangu Argentina iwapepete 1-0 na katika hatua ya 16-bora na kuwabandua.

Korea Kusini walipiku Uruguay kwa wingi wa mabao na kuambulia nafasi ya pili katika Kundi H baada ya kuokota jumla ya pointi nne.

Ureno walitawala kundi hilo kwa alama sita, tatu zaidi kuliko Ghana waliovuta mkia.

Wakitegemea zaidi maarifa ya Son Heung-min wa Tottenham Hotspur, Korea Kusini walifungua kampeni za Kundi H kwa sare tasa dhidi ya Uruguay kabla ya kukomoa Ghana 3-2 na kuangusha Ureno kwa mabao 2-1.

Kikosi hicho cha bara Asia kimewahi kusonga zaidi ya hatua ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia mara moja pekee.
Hiyo ilikuwa mwaka wa 2002 ambapo kilitinga nusu-fainali.

Kilikutana na Brazil mara ya mwisho mnamo Juni 2022 na kikakung’utwa 5-1 kirafiki.

Brazil watakaokosa huduma za wanasoka Gabriel Jesus, Alex Telles, Danilo Luiz da Silva na Alex Sandro kutokana na majeraha huku wakitegemea zaidi huduma za Neymar, Vinicius Jr, Richarlson Andrade na kipa Alisson Becker.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu afunzaye kwa kutumia nyimbo

Kiptum azoa Sh13m baada ya kushinda Valencia Marathon

T L