Brazil yaita kambini masogora wanane wanaopiga soka Uingereza kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia

Brazil yaita kambini masogora wanane wanaopiga soka Uingereza kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

BRAZIL wameteua masogora wanane wanaotandaza soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa ajili ya michuano ya Oktoba ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Hii ni licha ya Brazil kusalia katika orodha ya mataifa ambayo wakazi na raia wake wanazuiliwa kuingia Uingereza kutokana na ukali wa kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Mwezi uliopita, vikosi vingi vya EPL vilikataa kuachilia wachezaji walioitwa na timu za taifa kutoka Amerika Kusini kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Hali ilivyo kwa sasa, yeyote anayesafiri nchini Brazil kutoka Uingereza lazima aingie karantini kwa siku 14 pindi anapowasili Brazil na siku 10 anaporejea Uingereza.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Brazil limesema “mazungumzo chanya” yamefanywa kuhusiana na baadhi ya kanuni kali za kudhibiti usafiri.

Wanasoka wawili wa Liverpool Alisson Becker na Fabinho Henrique, Ederson Moraes na Gabriel Jesus wa Manchester City ni miongoni mwa wachezaji wa EPL watakaotegemewa na Brazil katika mapambano ya mwezi ujao kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia. Wengine ni beki Thiago Silva wa Chelsea, kiungo Fred wa Manchester United, fowadi Raphinha wa Leeds United na beki Emerson Royal wa Tottenham Hotspur. Wote hao wameitwa kambini kwa ajili ya michuano ijayo dhidi ya  Venezuela, Colombia na Uruguay.

Kiungo wa zamani wa Middlebrough, Juninho Paulista ambaye kwa sasa ni mratibu wa timu ya taifa ya Brazil, alisema wanasoka hao wanane wanaocheza kabumbu ya kulipwa nchini Uingereza wameitwa kambini kwa matumaini kwamba maafikiano kuhusu kulegezwa kwa kanuni za kusafiri kwa wachezaji yatapatikana wiki ijayo.

“Tumekuwa na vikao kadhaa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), vinara wa EPL na Serikali ya Uingereza. Tuna wingi wa matumaini kwamba suluhu ya kudumu itapatikana wiki ijayo. Hiyo ndiyo sababu tumewaita wanasoka hao kambini,” akasema Paulista.

Shirikisho la Soka la Brazil hata hivyo, litalazimika kuafikiana na mamlaka ya afya kuwaondoa wachezaji wanaotandaza kandanda ya kulipwa nchini Uingereza kwenye ulazima wa kutiwa karantini.

Mnamo Agosti 2021, vikosi vya EPL vilitoa taarifa kwamba vilikuwa vimeafikiana kwa pamoja kutoachilia wachezaji kurejea katika mataifa yaliyopigwa marufuku na Uingereza kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Septemba wakati wa likizo fupi iliyoshuhudia EPL ikipisha mechi hizo.

Hata hivyo, wachezaji wanne wakiwemo Emiliano Buendia na Emiliano Martinez wa Aston Villa, pamoja na Giovani lo Celso na Cristian Romero wa Tottenham, walisafiri nchini Argentina kuwa sehemu ya kikosi kilichovaana na Brazil kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Hata hivyo, mchuano huo ulitibuka baada ya dakika tano za mwanzo maafisa wa afya kutoka Brazil walipojitoma uwanjani kusitisha mechi kwa mdai kwamba wanasoka hao wa EPL walikuwa na ulazima wa kuingia karantini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Tope la Jubilee latesa Raila

Shirika la kutafutia wakulima soko lawahimiza kukuza mimea...