Michezo

BREKI! Chelsea yatupa uongozi dhidi ya Brighton

January 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BRIGHTON, Uingereza

KLABU ya Chelsea ilitupa uongozi ikipigwa breki na Brighton katika sare ya 1-1 katika mechi ya kusisimua ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Januari Mosi uwanjani Amex.

Chelsea ilikuwa imeshinda mechi zake zote tano dhidi ya Brighton ligini tangu Brighton iingie Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2017.

Vijana wa kocha Frank Lampard waliongoza dakika 45 za kwanza kwa bao moja lililofungwa na beki Mhispania Cesar Azpilicueta kabla ya mshambuliaji wa Iran, Alireza Jahanbakhsh kusawazisha katika dakika za lala-salama.

Mbrazil Willian alipiga kona safi ndani ya kisanduku cha Brighton, ambayo mshambuliaji matata Tammy Abraham alielekeza langoni, lakini ikazuiwa na kiungo Aaron Mooy kwenye laini kabla ya Azpilicueta kupata mpira vyema na kuujaza wavuni.

Raia wa Australia, Mooy alipumzishwa dakika ya 68 na nafasi yake kujazwa na Jahanbakhsh, ambaye pia alitikisa nyavu kutokana na kona iliokuwa imeondoshwa vibaya na Chelsea.

Matokeo haya yameshuhudia Chelsea ikijiongezea alama moja na kufikisha jumla ya alama 36 kutokana na mechi 21. Chelsea inasalia katika nafasi ya nne na ya mwisho ya kufuzu kushiriki Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Iko nyuma ya Liverpool inayioongoza kwa alama 55, Leicester (42) na mabingwa watetezi Manchester City (41).

Alama moja nayo ilitosha kusukuma Brighton nafasi moja juu hadi nafasi ya 13.

Brighton imevuna alama 24 sawa na Burnley, ambayo ilikubali kichapo cha tatu mfululizo hapo jana na kuteremka chini nafasi moja.

Baada ya kuchabangwa na Everton na Manchester United katika mechi zake mbili za mwisho za mwaka 2019, Burnley ilifungua mwaka 2020 kwa kuzamishwa 2-1 na Aston Villa kupitia mabao yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza kutoka kwa Wesley na Jack Grealish.

Burnley ilijifariji na bao kutoka kwa Chris Wood ambalo lilifungwa dakika ya 80.

Leo Alhamisi itakuwa zamu ya Liverpool kuzichapa dhidi ya washiriki wapya Sheffield United uwanjani Anfield.

Katika mechi hii, vijana wa kocha Jurgen Klopp watakuwa mawindoni kudumisha rekodi ya kutoshindwa nyumbani hadi mechi 51 na hawajashindwa na timu zilizopandishwa daraja katika mechi 14 zilizopita.