Habari Mseto

Breki kwa ada mpya ya nyumba kukatwa kwa mishahara

December 20th, 2018 1 min read

ABIUD ACHIENG na RICHARD MUNGUTI

MPANGO wa Serikali kuwatoza wafanyakazi wote wa umma na walio katika sekta ya kibinafsi ada ya asilimia 1.5 kugharamia ujenzi wa makazi ulisitishwa na mahakama kuu jana.

Serikali ilikuwa imetoa mwongozo kwamba ada hiyo ianze kulipwa na wafanyakazi wote kuanzia Janauri 2019.

Jaji Hellen Wasilwa alisitisha utekelezaji wa mpango huo aliposikiza kesi iliyowasilishwa na katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu) Bw Francis Atwoli.

Bw Atwoli alipinga kutekelezwa kwa mpango huo akisema mashauri hayakufanywa kabla ya agizo kutolewa na Serikali wafanyakazi wote wachangie katika hazina ya ujenzi wa makazi mazuri kwa bei nafuu.

Jaji Wasilwa aliyeratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura aliamuru maagizo ya kusitisha malipo hayo ya asilimia 1.5 yatasalia hadi pale kesi hiyo ya Bw Atwoli itakaposikizwa na kuamiliwa.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya Kifungu nambari 31A cha sheria uajiri ya 2007 kilichoambatanishwa na Sheria za Hazina ada hiyo ilikuwa ianze kulipwa Januari 1,2019.

Lakini Cotu inayowatetea wafanyakazi 2.5milioni ilisema ada hiyo itaathiri mapato ya wengi.

Wakili aliyewakilisha Cotu Bw Okweh Achiando alisema kutekelezwa kwa ada hiyo kutasababisha kila mfanyakazi alipe pesa sisizopungua Sh5, 000.

Bw Achiando alisema kuwa ada hiyo itavuruga familia nyingi ambazo wanaofanya kazi hupokea mishahara duni.

Alisema chini ya sheria za leba kila mfanyakazi anastahili kupata mshahara mzuri utakaomwezesha kukidhi maisha yake.

Jaji aliamuru Waziri wa Fedha , Waziri wa Uchukuzi wapewe nakala za kesi hiyo ndipo wajibu madai kuwa wamekandamiza wafanyakazi.

Kesi hiyo itasikizwa Janauri 1, 2019