Makala

BRENDA ACHIENG': Usikubali kutafunwa na maprodusa mafisi

November 24th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ANAWAPONDA maprodusa ambao hupenda kuwashusha hadhi wasanii wanaoibukia hasa wa kike kwa kuwatumia ili kuwapa ajira na kuwatema.

Aidha anashauri wenzake wajipende, wajiheshimu wala wasikubali kutumiwa na maprodusa mafisi.

Kadhalika Brenda Achieng ambaye ni kati ya waigizaji wanaokuja kwenye gemu anasema lazima wakaze buti mjengoni.

“Ni vyema kusubiri muda mwafaka utakapotimia kuliko kujishusha hadhi ili kupata umaarufu haraka,” alisema na kuongeza kuwa sekta ya masuala ya burudani imegubikwa na vituko visivyofaa.

Ingawa alitamani kuwa mwanamaigizo tangia akiwa mtoto alipata motisha zaidi alipotazama filamu iitwayo ‘Quantico’ kazi yake mwigizaji Priyanka Chopra mzawa wa India.

Kando na uigizaji Priyanka Chopra aliwahi kunasa tuzo la Miss World 2000 Pageant ni prodyuza wa filamu na muimbaji.

Hata hivyo kisura huyu anashiriki maigizo huku akilenga kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo. Anasema anatamani sana kufikia kiwango cha waigizaji kama Priyanka Chopra pia Scarlett Johansson mzawa wa Marekani.

Ingawa alianza kujituma katika masuala ya uigizaji mwaka 2016 anasema kazi aliyowahi kushiriki ‘Why Hate?’ ni kati ya filamu zilizowahi kupendeza zaidi.

Msichana huyu anajivunia kufanya kazi na makundi mbali mbali tangia aanze uigizaji. Amefanya na Informatrix Arts Production, Starlight Production na kwa sasa anaendelea kukuza talanta yake chini ya kundi la Badilisha Arts lenye makazi yake katika mtaa wa Kayole, Kaunti ya Nairobi.

Anayataka mashirika yanayomiliki vyombo vya habari kuanzisha vipindi vingi kupeperusha filamu za humu nchini ili kutoa ajira kwa wasanii chipukizi. Picha/ John Kimwere

Changamoto

Kando na kuwa wanaouwezo wa kufanya vizuri katika sekta ya maigizo anasema wasanii wengi hasa wa kike hunyimwa nafasi za ajira kwa kutojulikana.

”Kando na hilo suala la ubaguzi limetawala jukwaa ya uigizaji ambapo baadhi yetu hujikuta njiapanda bila kutarajia,” anasema.

Anahimiza Wakenya wawache kupuuza filamu za waigizaji wazalendo bali wawe mfano mwema kwa kuwapa sapoti ili kuwatia motisha zaidi kukuza vipaji vyao.

”Ni muhimu wazalishaji wa filamu hapa nchini tuwe wabunifu pia tuegemee zaidi utamaduni wetu,” alisema na kuongeza kuwa anahisi hatua hiyo itavutia wapenzi wa burudani ya maigizo wa humu nchini.

Anadokeza kuwa Wakenya wengi hupenda kutazama filamu za kigeni maana wahusika wamekuwa katika mstari wa mbele kutangaza utamaduni wao kinyume na ilivyo hapa Kenya.

Anatoa mwito kwa wasanii wanaokuja kwenye gemu wafahamu uigizaji siyo mteremko unahitaji nidhamu, kujitolea na kujituma bila kulegeza kamba pia kumtegemea Mungu zaidi. Pia anawaambia kamwe wasipuuze masomo maana ndiyo msingi wa kila jambo wanalofanya.

Kadhalika anawashauri wafanye utafiti zaidi kuhusu masuala ya uigizaji hasa wale wanaolenga kubobea katika taaluma ya maigizo.