Makala

BRENDA BOSIBORI: Sanaipei Tande hunitia moyo

August 24th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

INGAWA hajapata mashiko katika masuala ya muziki wa burudani amepania kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha anafikia viwango vya kimataifa miaka ijayo. Hakika ni miongoni mwa wasanii wa kike wanaokuja wanaopania kuvumisha sekta ya muziki wa densi.

Binti huyu anaorodheshwa kati ya wanamuziki na waigizaji wanaokuja katika tasnia ya burudani. Alitambua talanta yake katika ya muziki mwaka 2015 baada ya kukamilisha masomo ya Upili katika Shule ya St. Peters Suneka, Kaunti ya Kisii.

Brenda Bosibori maarufu Suby ni mwanafunzi wa mwaka wa pili kwenye Chuo Kikuu cha Multimedia (MMU) anakosomea kuhitimu kwa shahada ya Diploma katika masuala ya uhusiano mwema.

”Binafsi ninaamini nina uwezo tosha kutoa nyimbo nzuri za kutikisa zaidi katika ulingo wa muziki wa burudani hapa nchini na Afrika Mashariki kwa jumla,” alisema na kuongeza kwamba ukosefu wa ufadhili ndiyo changamoto kubwa kwa wanamuziki wengi.

MAREKANI

Mwanamuziki huyu aliyezaliwa mwaka 1995 hughani nyimbo ambazo huzungumzia masuala ya mapenzi, mazingira na maisha kwa mitindo tofauti ikiwamo Zuku, Reggae na Hip hop. Katika mpango mzima anasema amepania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha anatinga kiwango cha mwanamuziki mahiri mzawa wa Marekani, Tatiana Manaois.

Kisura huyu anajivunia kutunga, kurekodi na kuachia jumla ya nyimbo saba zikiwamo tano-Video na mbili-Audio. Baadhi ya fataki ambazo amefaulu kutunga kama:’Ajabu,’ ‘Oyomo,’ ambazo ameshirikisha msanii wa kiume Mokua Obed maarufu kama DJ O.

Nyimbo nyingine ikiwa ‘Mazingira,’ ambayo amewashirikisha wasanii Rafat chizi, DJ O na Everedi pia ‘Barua’ ambazo zimerekodiwa kwenye studio itwaayo KBM Records.

Hata hivyo kwa sana anasema hufanya kazi na studio kwa jina Asali Productions inayopatikana eneo la Embakasi awali ikifahamika kama Bligs Media Prodution. Kadhalika amerekodi cover song iliyotungwa na mwanamuziki Bensoul iitwayo ‘Never forget You’ na ‘Helpless’ ambayo ndiyo nyimbo ya kwanza kurekodi.

SCRIPT

Katika masuala ya maigizo anajivunia kuwa mwandishi anayeibukia wa Script ambapo mwaka 2018 aliandika filamu moja iitwayo ‘Liberty Theatre’ iliyoishia kuonyeshwa kwenye ukumbi wa Kenya National Theatre (KNT). ”Ninahisi nina talanta ya kuandika filamu ambapo kwa sasa ninaendelea kuandikisha nyingine itakayojulikana kama ‘Sisi.’

SANAIPEI TANDE

Kwa wasanii wa hapa Kenya, kisura huyu anasema angependa kuwapiku wasanii kama Sanaipei Tande mtunzi wa nyimbo kama ‘Najuta,’ na ‘Chaguo la Moyo,’ kati ya zingine.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki anapania kufikia kiwango cha Nandy ambaye ni miongoni mwa mwanamuziki wa kike wa Bongo Fleva. Hapa Kenya anasema anagependa kufanya kazi na wasanii kama:Avril na Sanaipei Tande kati ya wengine.

Binti huyu anashauri wasanii wenzie wanaokuja kwamba wanahitaji kuwa makini na wavumilifu ili kufanya vizuri katika tasnia ya muziki. Anasema huwa inasikitisha sana msanii kurekodi nyimbo yake na kabla ya kuiachia kuipata madukani ikiuzwa.