Brenda Ochieng anavyotesa katika tasnia ya uigizaji

Brenda Ochieng anavyotesa katika tasnia ya uigizaji

Na JOHN KIMWERE

PENGINE sura na jina lake sio geni kwa wapenzi wa tasnia ya filamu hapa nchini. Ingawa ni miaka mitatu sasa tangia aanze kujituma kwenye masuala ya maigizo anajivunia kuchota wafuasi wengi tu ambao humfuatilia kwa vipindi tofauti ambavyo hupeperushwa kupitia runinga mbali mbali nchini.

Anasema amepania kujituma bila kulaza damu huku akidhamiria kutinga upeo wa filamu za kimataifa, Hollywood na kuibuka staa mahiri duniani.

Brenda Anyango Ochieng ameorodheshwa kati ya wanadada wanaozidi kuvumisha tasnia ya uigizaji nchini. Kando na uigizaji dada huyu ni meneja pale Klick Studio Buruburu, Nairobi.

VIOLA DAVIS

”Ingawa tangia nikiwa mdogo nilitamani kuhitimu kuwa wakili ama mwanahabari kipaji changu katika uigizaji kilitambuliwa na Innocent Muga aliyekuwa mwalimu wangu nikisoma kidato cha pili,” alisema na kuongeza kuwa kipindi hicho alishauriwa kujiunga na kundi la drama shuleni.

Anasema hatua ya kuanza kujihusisha na masuala ya uigizaji ilichochewa pakubwa baada ya kutazama filamu iitwayo ‘Windows’ kazi yake mwigizaji mahiri, Viola Davis mzawa wa Marekani. Katika mpango mzima anasema ndani ya miaka mitano ijayo analenga kuibuka kati ya waigizaji maarufu Afrika huku akiwa katika mstari wa mbele kukuza talanta za wasanii wanaoibukia.

Mwigizaji huyu ambaye mwanzo wake alianza kushiriki filamu chini ya kundi la Moonbeam Productions mwaka 2018 anasema kwake uigizaji ni ajira. Aidha anasema anajivunia kufanya kazi na makundi mengine kama; Phili It Tv, Njugush Creative, Multan Productions, SK Productions, Giraffe Africa Productions, Allison Productions bila kusahau Tag Team.

AUNTIE BOSS

Katika mpango mzima anajivunia kushiriki zaidi ya filamu kumi ndani ya kipindi cha miaka mitatu. Baadhi yazo zikiwa:’Auntie boss (Maisha Magic East na NTV),’ ‘Masaibu ya Njugu (NTV),’ ‘Sweet Moyo(Youtube),’ na ‘Andakava,’ ‘Njoro wa Uba,’ ‘Varshita,’ ‘Selina,’ na ‘Hullabaloo Estate,’ (Zote Maisha Magic East) kati ya zingine.

”Katika uigizaji ninalenga kujituma mithili ya mchwa huku nikipania kufikia upeo wa wanamaigizo shupavu duniani akiwamo Viola Davis bila kumsahau Mkenya anayetamba katika filamu za Hollywood, Lupita Nyong’o.” Viola Davis anafahamika kutokana na filamu zake kama ‘Suicide Squad,’ na ‘Prisoners’ naye Lupita alipata umaarufu kufuatia filamu kama ’12 Years a slave,’ na ‘Black Panther.”

Kwa wasanii ambao hushiriki maigizo humu nchini anasema angependa sana kufanya kazi nao Kate Actress na Victoria Mzenge. Kimataifa anadokeza kuwa angependa sana kujikuta jukwaa moja na Mkenya, Lupita Nyong’o pia Elia Thomas mzawa wa Eritrea.

MAWAIDHA

Anashauri wana dada wanaoibukia kuwa wasiwe na pupa ya kuibuka mastaa katika tasnia ya maigizo. Anasema itakuwa vyema kwa wanadada kuwakwepa wanaume ambao hupenda kuwashusha hadhi kwa kuwataka kimapenzi ili kuwapa ajira. Aidha anawahimiza kuwa nyakati zote wanastahili kujiheshimu pia kumweka Mungu mbele kwa chochote wanachofanya.

You can share this post!

Shalom Yassets inavyookoa vijana mitaani

Deby azikwa huku jeshi la nchi likigawanyika kuwili