Kimataifa

#Brexit yatishia kuzua uhaba wa shahawa Uingereza

August 27th, 2018 1 min read

MASHIRIKA NA PETER MBURU

HUENDA kujiondoa kwa nchi ya Uingereza kutoka Muungano wa Ulaya (EU) , Brexit, kukawa na athari ambazo hazikutarajiwa, zikiwemo kuadhiri vizazi vijavyo.

Wananchi wengi wa UK wamekuwa wakitumia mbinu za kisasa (artificial insemination) kupata watoto, na hivyo taifa hilo limekuwa likipata vifaa vya kuhifadhi shahawa (sperm banks) kutoka mataifa ya nje, yaliyo katika muungano wa EU.

Sasa ikiwa UK itajiondoa na sheria za sasa kuanza kufanya kazi, manii pamoja na vifaa vya kuyahifadhi havitauziwa UK tena na mataifa ya EU, ili kuwezesha watu kuzidi kupata watoto kwa njia za kisayansi.

Kulingana na ripoti za serikali zilizochapishwa Alhamisi, Uingereza ilipokea takriban sampuli 3,000 za manii kutoka hifadhi yake nchini Denmark mwaka uliopita, na sampuli 4,000 kutoka Marekani.

Hata hivyo, usambazaji wa shahawa hivyo umeenda chini tangu wafadhili waathiriwe na sheria mpya ambayo haijawapa usiri.

Uingereza aidha imekuwa ikipokea mayai ya wanawake pamoja na viumbe vya watoto kutoka mataifa ya EU, yakifikia 500 mwaka jana.

Ikiwa mazungumzo ya kuokoa Brexit hayatafaulu, serikali ilisema sheria ya sasa inayoelekeza kuhusu kuingizwa kwa manii itakwaza, huku sheria za EU zikiwa hazitafanya kazi Uingereza tena.

Hali hiyo sasa inasemekana kuzidisha hofu miongoni mwa wanandoa Uingereza, wakihofia kuhusu uzazi wa siku zijazo.