Brighton na Arsenal waumiza nyasi bure katika mechi ya EPL ugani Amex

Brighton na Arsenal waumiza nyasi bure katika mechi ya EPL ugani Amex

Na MASHIRIKA

KOCHA Graham Potter amesema ujasiri ulioonyeshwa na vijana wake katika sare tasa iliyosajiliwa na Brighton dhidi ya Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi ugani Amex ni ishara ya uthabiti wa kikosi hicho.

Brighton almaarufu The Seagulls walionekana kuwazidi Arsenal maarifa katika takriban kila idara japo wakashindwa kutumia vyema nafasi kadhaa za wazi walizozipata katika kipindi cha kwanza kupitia Dan Burn, Leandro Trossard, Neal Maupay, Shane Duffy na Pascal Gross.

“Tulijaribu kila kitu. Naamini mashabiki walifurahia sana mechi hiyo kwa sababu tulionyesha ukakamavu japo tulikosa alama tatu muhimu,” akasema Potter.

Fursa ya pekee ya kufunga ambayo Arsenal ya kocha Mikel Arteta ilipata katika kipindi cha kwanza ni jaribio la Pierre-Emerick Aubameyang aliyepania kukamilisha krosi ya Bukayo Saka.

Kombora la kiungo mvamizi Emile Smith Rowe lilidhibitiwa kirahisi na kipa wa Brighton, Robert Sanchez. Matokeo hayo yalisazwa Brighton katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama 14 sawa na Manchester United, Liverpool na Everton waliowalazimishia Man-United sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya EPL mnamo Jumamosi.

“Huu ni msingi thabiti tunaojitahidi kuweka kikosi. Alama 14 kutokana na mechi saba ni mwanzo mzuri kwa Brighton ligini. Muhimu zaidi kwa sasa ni kuendeleza ukakamavu huo kwa sababu matokeo ya hadi sasa yanatuaminisha zaidi,” akasema Potter.

Arsenal walijibwaga ugani kwa ajili ya mechi hiyo wakipigiwa upatu wa kushindi ikizingatiwa ubora wa matokeo yao katika mechi ya awali iliyowapa ushindi wa 3-1 dhidi ya Tottenham Hotspur.

Ingawa Brighton walielekeza makombora 21 langoni mwa Arsenal, ni mawili pekee kati ya hayo yalionekana kumtatiza kipa Aaron Ramsdale, 23.

Ni Manchester City na Chelsea pekee ambao wanajivunia rekodi ya kupiga jumla ya mechi tisa za EPL bila ya kufungwa katika viwanja vyao vya nyumbani mwaka huu wa 2021. Brighton kwa upande wao wamesakata michuano minane bila kufunga bao ugani Amex.

Arsenal wamepachika wavuni mabao matano pekee katika mechi saba za ufunguzi wa msimu huu, hiyo ikiwa idadi ya chini zaidi kufikia hatua kama hii ya msimu tangu 1986-87.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea wapepeta Southampton na kupaa hadi kileleni mwa...

UDAKU: Ma’ Rashford mbioni kupatanisha mwanawe na mrembo...