Michezo

Brighton waaibisha Newcastle United nyumbani kwao

September 21st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

NEAL Maupay alifunga mabao mawili na kusaidia Brighton kuwapepeta Newcastle United 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha uwanjani St James’ Park mnamo Septemba 20, 2020.

Brighton almaarufu ‘Seagulls’ walitumia gozi hilo kama jukwaa bora la kujinyanyua baada ya kupoteza mechi yao ya kwanza ya msimu huu dhidi ya Chelsea kwa mabao 3-1 mnamo Septemba 14.

Maupay aliwaweka Brighton kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya nne ya kipindi cha kwanza baada ya Tariq Lamptey kuchezewa visivyo na Allan Saint-Maximin.

Bao la pili la Maupay lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Leandro Trossard katika dakika ya saba.

Newcastle walizidiwa maarifa katika takriban kila idara na hawakuelekeza kombora lolote lililolenga shabaha kwa upande wa Brighton hadi dakika ya 40.

Baada ya fataki ya Trossard kubusu mhimili wa lango la Newcastle, Brighton walizamisha kabisa chombo cha wenyeji wao kupitia kwa Aaron Connolly aliyefunga bao la tatu katika dakika ya 83.

Yves Bissouma alionyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa mechi hiyo kwa kumchezea vibaya kiungo Jamal Lewis wa Newcastle waliowapiga West Ham United 2-0 katika mechi ya kwanza ya EPL mnamo Septemba 12.

Ushindi huo wa kwanza wa Newcastle uliwachochea kuwapepeta Blackburn Rovers 1-0 katika raundi ya pili ya Carabao Cup mnamo Septemba 15, 2020.

Baada ya kuvaana na Morecambe katika raundi ya tatu ya EFL Carabao Cup mnamo Septemba 23, Newcastle wamepangiwa kuvaana na Tottenham Hotspur, Burnley na Manchester United kwa usanjari huo.

Kwa upande wao, Brighton watavaana na Preston katika raundi ya tatu ya EFL Cup mnamo Septemba 23 kabla ya kukabiliana na Man-United, Everton na Crystal Palace kwa usanjari huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO