Michezo

Brighton yazika matumaini ya Arsenal kutinga Nne Bora

June 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NEAL Maupay alifunga bao mwishoni mwa dakika tano za ziada na kusaidia Brighton kusajili ushindi muhimu wa 2-1 dhidi ya Arsenal uwanjani American Express mnamo Juni 20, 2020.

Bao hilo lilikuwa la tisa kwa mfumaji huyo mzawa wa Ufaransa kupachika wavuni hadi kufikia sasa kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Ushindi wa Brighton ulikuwa wao wa kwanza mwaka huu wa 2020 na huo ulikuwa mchuano wa kwanza kuwashuhudia wakitoka nyuma na kusajili ushindi katika mechi ya EPL muhula huu.

Nicolas Pepe aliwaweka Arsenal kifua mbele kunako dakika ya 70 kwa kutumia guu lake la kushoto kuvurumisha wavuni kombora zito nje ya eneo la hatari. Ingawa goli hilo lilionekana kuwapa Arsenal alama tatu muhimu, Brighton walirejeshwa mchezoni na Lewis Dunk aliyesawazisha kunako dakika ya 75 baada ya kizaazaa kutokea langoni pa The Gunners.

Goli la Maupay liliwatoa Arsenal pumzi zaidi hasa ikizingatiwa kwamba hiyo ilikuwa mechi yao ya pili mfululizo kupoteza tangu kurejelewa kwa kampeni za EPL mnamo Juni 17, 2020.

Ni matokeo ambayo yalididimiza kabisa matumaini ya Arsenal ya kumaliza kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Chini ya mkufunzi Mikel Arteta, Arsenal walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi dhidi ya Brighton wakitarajiwa kutawaliwa na hamasa ya kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa kwa mabao 3-0 kutoka kwa Manchester City mnamo Juni 17.

Hata hivyo, hamasa na kiu ya kupata ushindi ni jambo ambalo lililokosekana kabisa katika kikosi cha Arsenal. Pigo zaidi kwa kikosi cha Arteta huenda ni ulazima wa kusakata mechi zote zilizosalia msimu huu katika EPL na Kombe la FA bila ya huduma za kipa chaguo la kwanza, Bernd Leno aliyeondolewa uwanjani katika kipindi cha kwanza baada ya kupata jeraha la kiufundo cha mguu alipokuwa akikabiliana na Maupay ndani ya kijisanduku.

Tukio hilo lilionekana kuwakera zaidi baadhi ya wanasoka wa Arsenal waliomrushia Maupay cheche za maneno na kuonekana kusukumana naye wakiondoka uwanjani mwishoni mwa mchezo.

Leno kwa sasa anajumuika mkekani na beki Pablo Mari na kiungo Granit Xhaka waliopata majeraha wakati wa mechi dhidi ya Man-City.

Ushindi kwa Brighton uliwapaisha kwenye msimamo wa jedwali hadi nafasi ya 15 kwa alama 32, nne zaidi kuliko Watford ambao pia walitoka nyuma mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwalazimishia Leicester City sare ya 1-1 mnamo Juni 20.

Kwa upande wao, Arsenal wangali na alama 40, mbili nyuma ya Tottenham Hotspur ambao pia waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Manchester United katika mchuano mwingine wa EPL mnamo Juni 19.

Kibarua kikubwa zaidi kwa Brighton sasa ni kuendeleza ubabe wanaohitaji dhidi ya klabu zinazofunga orodha ya 10-bora jedwalini katika jumla ya mechi nane zilizosalia. Wamepangiwa kuvaana na Leicester uwanjani King Power mnamo Juni 23.