Michezo

Brigid Kosgei avunja rekodi ya Marathon duniani

October 14th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Brigid Kosgei na Lawrence Cherono walitawala mbio za kifahari Jumapili za Chicago Marathon nchini Amerika, huku Kosgei akivunja rekodi ya dunia ya wanawake ya Paula Radcliffe ya saa 2:15:25 iliyokuwa imedumu tangu mwaka 2003.

Kosgei alinyakua taji lake la pili mfululizo la Chicago kwa saa 2:14:04 katika mbio hizi zilizovutia watimkaji 45,000.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 25 aliongoza mbio hizi kutoka mwanzo hadi utepeni.

Alivunja pia rekodi ya dunia ya wanawake pekee ya saa 2:17:01 ambayo Mkenya mwenzake Mary Keitany aliweka jijini London mwaka 2017.

Alifuta rekodi ya Chicago Marathon ya wanawake ya saa 2:17:18 ambayo Radcliffe aliweka mwaka 2002.

Naye Cherono alimaliza ukame wa Kenya wa miaka miwili bila taji la wanaume la Chicago alipobeba taji kwa saa 2:05:45.

Alimaliza sekunde moja mbele ya raia wa Ethiopia, Dejene Debela naye Asefa Mengstu akafunga msururu wa tatu-bora (2:05:48).

Kosgei alifuatwa dakika sita baadaye na Waethiopia Ababel Yeshaneh (2:20:51) na Gelete Burka (2:20:55). Mwuingereza Radcliffe alitimka 2:15:25 katika London Marathon mwezi Aprili mwaka 2003.

Kosgei, ambaye alishinda London Marathon mwezi Aprili 2019 alikuwa ameapa kufuta rekodi ya Radcliffe mjini Chicago.