Habari Mseto

Bruno aifungia United penalti

June 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

PAUL Pogba aliwajibishwa kwa mara ya kwanza tangu Disemba 26, 2019 katika mechi iliyomshuhudia akitokea benchi na kusababisha penalti iliyowapa Manchester United sare ya 1-1 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 19, 2020

Pogba ambaye hakuwa amechezeshwa kwa takriban miezi sita kutokana na jeraha lililomhitaji kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu, aliingia ugani katika kipindi cha pili na kuongeza ubunifu kwenye safu ya kati ya Man-United.

Penalti ya Man-United, ambayo ilifungwa na kiungo Bruno Fernandes, ilikuwa zao la Pogba kukabiliwa vibaya na beki Eric Dier wa Tottenham.

Alama moja iliyotiwa kapuni na Man-United iliwasaza katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama 46, nne zaidi kuliko Tottenham ambao pia wanapigania fursa ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Goli la Tottenham lilifumwa wavuni kupitia kwa Steven Bergwijn kunako dakika ya 27. Kombora la kiungo huyo mzawa wa Uholanzi lilimbabatiza kipa David de Gea aliyesalia kujilaumu kutokana na masihara yake.

Bao la Fernandes kunako dakika ya 81 liliwarejesha Man-United mchezoni kiasi kwamba walikita kambi langoni pa wenyeji wao na nusura wafunge la pili kupitia penalti nyingine iliyobatilishwa na refa Jon Moss baada ya kurejelewa kwa teknolojia ya video ya VAR.

Baada ya kutambua makosa yake, De Gea alilazimika kufanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Son Heung-min huku juhudi sawa na hizo zikishuhudiwa kutoka kwa kipa Hugo Lloris aliyewanyima Fernandes, Anthoy Martial na Marcus Rashford nafasi nyingi za wazi.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer alikidumisha kikosi kilichopiga mfululizo wa mechi 11 bila kupoteza hata moja katika mapambano yote ya msimu huu hadi soka ya Uingereza ilipositishwa kwa muda mnamo Machi 13, 2020 kutokana na janga la corona.

Mchuano dhidi ya Man-United uliwapa Tottenham jukwaa maridhawa la kukaribisha kikosini nahodha Harry Kane aliyekuwa amefanyowa upasuaji wa paja na fowadi Son aliyevunjika mkono mwishoni mwa mwaka uliopita. Tottenham kwa sasa wanajiandaa kwa gozi la London litakalowashuhudia wakiwa wenyeji wa West Ham United mnamo Juni 23, siku moja kabla ya  Man-United kualika Sheffield United uwanjani Old Trafford.

MATOKEO YA EPL (Ijumaa):

Norwich City 0-3 Southampton

Tottenham 1-1 Man-United