Bruno Fernandes aweka rekodi EPL

Bruno Fernandes aweka rekodi EPL

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata wa Manchester United na timu ya taifa ya Ureno, Bruno Fernandes, ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwezi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya nne chini ya kipindi cha mwaka mmoja.

Hii ni baada ya sogora huyo kutwaa taji hilo kwa mara nyingine mnamo Disemba 2020 na kuifikia rekodi iliyowekwa na nyota Cristiano Ronaldo, ambaye pia ni Mreno, wakati akivalia jezi za Man-United kabla ya kuyoyomea Uhispania kuchezea Real Madrid.

Hakuna mwanasoka mwingine ambaye amewahi kutia kapuni mataji manne ya Mchezaji Bora wa Mwezi katika EPL chini ya kipindi cha miezi 12.

Mnamo Disemba, Fernandes alifunga jumla ya mabao matatu na kuchangia mengine matatu katika ufanisi uliosaidia Man-United almaarufu ‘The Red Devils’ kupaa hadi kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 36 kutokana na mechi 17.

Fernandes kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 11 ya EPL kapuni mwake na amechangia saba mengine kufikia sasa muhula huu.

Alipokezwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Disemba baada ya kuibuka mshindi katika miezi ya Februari, Juni na Novemba 2020.

Kwa kuibuka mshindi wa taji hilo mnamo Disemba, Fernandes sasa anakuwa mchezaji wa kwanza kunyanyua ubingwa huo mara mbili mfululizo baada ya Mohamed Salah wa Liverpool mnamo Februari na Machi 2018.

Sergio Aguero wa Manchester City ndiye ametawazwa mshindi wa taji hilo mara nyingi zaidi baada ya kutangazwa mfalme mara saba.

Hata hivyo, Fernandes, 26, angali na muda zaidi wa kufikia na hata kuipita rekodi ya Aguero ambaye ni raia wa Argentina.

Aliyekuwa mwanasoka matata wa Liverpool, Steven Gerrard, na Harry Kane wa Tottenham Hotspur wanashikilia nafasi ya pili baada ya kila mmoja kutawazwa mshindi mara sita.

Nyota wa zamani wa Man-United Robin van Persie na Wayne Rooney wanashikilia nafasi ya nne kwa pamoja baada ya kila mmoja wao kutwaa taji la Mchezaji Bora wa Mwezi katika EPL mara tano. Rooney alistaafu rasmi kwenye ulingo wa usogora baada ya miaka 19 mnamo Ijumaa na kupokezwa mikoba ya kuwatia makali vijana wa kikosi cha Derby nchini Uingereza.

Rooney, 35, ndiye mfungaji bora wa muda wote katika timu ya taifa ya Uingereza (mabao 53) na ndiye anaongoza orodha ya wafungaji bora wa Man-United (mabao 253).

Kurejea kwa Man-United kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kubanduliwa mapema msimu huu ni zao la mchango mkubwa wa Fernandes – nyota aliyesajiliwa kutoka Sporting Lisbon kwa kima cha Sh9.5 bilioni mnamo Januari 2020.

Ujio wa Fernandes umekuwa kiini cha ufufuo wa makali ya Man-United ambao kwa sasa wanapigiwa upatu wa kutwaa taji la EPL chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Boit, Kandie kujaribu kubwaga Cheptegei na Mo Farah Olimpiki

MIAKA 40: Museveni ashinda urais kwa mara ya sita mfululizo