Dondoo

Buda afurusha bintiye kwa kuvaa suruali ya kubana

March 28th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KIZAAZAA kilizuka katika boma moja la hapa baada ya mzee kumtimua binti yake alipofika nyumbani kutoka chuoni akivalia kaptula fupi mno jambo lililomkasirisha mzee.

Kulingana na mdokezi, kipusa alipofika kwao, alienda moja kwa moja akitaka kumpa pambaja baba yake.

Inadaiwa mzee alikataa kumkumbatia binti yake. “Kama ni salamu unataka kunipa kaa nazo. Sizihitaji kwa sasa,” mzee alimkaripia bintiye.

Mwanadada alishangaa. Alielekea alikokuwa mama yake na mzee akamfuatisha maneno. “Unatoka wapi ukiwa umevalia hivi?” mzee alimuuliza binti yake kwa ukali.

Duru zinasema mama ya kipusa alijaribu kumshawishi mzee apunguze hasira lakini hakutoboa.

“Nimeuliza anatoka wapi akiwa amevaa hivi? Huyu hatakaa hapa kwangu. Arudi atokako. Angalia, uchi wake wote uko nje,” mzee alimkemea binti yake.

Inadaiwa kipusa aliamua kujitetea kwa kumueleza mzee kwamba huo ndio mtindo wa mavazi chuoni.

“Kuvalia suruali fupi inayokubana mpaka nyama zote za mwili ziko nje ndio mtindo unaoniambia. Kwangu hutakaa,” mzee aliapa.

Kulingana na mdokezi, mzee alimpa binti yake dakika kumi abadilishw nguo hiyo au arudi shuleni alikotoka. Alipoona mrembo hakushtuka, mzee aliamua kumtimua.

“Hicho kiingereza chako na kaptula yako vipeleke kwingine. Mamako tangu nimuoe, hajawahi kuvaa hivi. Umenikosea heshima kabisa. Labda mimi si baba yako,” mzee alichemka huku akimtimua binti yake.

Inadaiwa mzee alitoa fimbo na kumuamrisha mrembo kuondoka boma lake naye akalazimika kukimbilia usalama wake.

“Kwenda kabisa. Hata masomo yako siyahitaji kwangu. Siku nyingine ukitoka masomo usikanyage hapa,” mzee alimkaripia binti yake.

…WAZO BONZO…