Dondoo

Buda akiri kanisani anakaranga yaya na mkewe kwa kikaango kimoja

May 31st, 2018 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MUNYU, THIKA

KIOJA kilishuhudiwa katika kanisa moja mtaani hapa mzee aliyeokoka alipokiri kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na yaya.

Inasemekana mkewe alikuwa akijaribu juu chini jamaa aokoke ili awe akiandamana naye kanisani kwa miaka 17 iliyopita. Hivi majuzi, ilikuwa furaha kwa mama huyo maombi yake yalipojibiwa na jamaa akaokoka.

“Huyu ndiye Mungu ninayemuomba kila siku, umekaribishwa sana kanisani mume wangu,” mkewe alisema akitabasamu.

Wakiwa kanisani mama aliketi karibu na mumewe uso wake ukionekana kujawa tabasamu. Misa ilianza na kuendeshwa kwa utaratibu.

Pasta alilisha kondoo wake chakula cha kiroho, ukawadia muda wa kutaka aliyeamua kukabidhi maisha yake kwa Mwenyezi Mungu ajitokeze.

Jamaa alinyanyuka na kuombewa. Hata hivyo, aliomba apewe dakika kadhaa ashukuru. “Kwa hakika niko mahala hapa kwa juhudi za mke wangu mpendwa. Nina ujumbe ambao ningeomba kumpasha,” jamaa alisema kanisa likitulia.

Alijipa dakika mbili hivi na hatimaye akapasua mbarika.

“Kuanzia leo nimekuwa mtu mpya, ambaye ameamua kumfuata Yesu Kristo. Maisha yangu ya awali yalikuwa yenye maovu tele, ninaomba kwa dhati mke wangu anisamehe kwa kuwa na uhusiano haramu na yaya. Ni jambo ambalo limekuwa likinikereketa maini,” alifichua.

Hata hivyo, yasemekana mkewe alikasirika, akasonga mbele na kumshika mashati. “Haiwezekani, iweje ufanye ukorofi huo? Yaani umekuwa ukinikaanga chungu kimoja na mjakazi wa nyumbani?” mama alitaka kujua.

Mama huyo alitishia kumpa polo talaka lakini pasta akamtuliza akimwambia tayari jamaa alikuwa kiumbe kipya.

Aliita kikaokilichojumuisha wazee wa kanisa, na haikufahamika kilichojadiliwa.

…WAZO BONZO…