Buda aliyefumaniwa alipa Sh0.5m

Buda aliyefumaniwa alipa Sh0.5m

Na MWANDISHI WETU

KAGIO, KIRINYAGA

BUDA eneo hili alilazimika kulipa mwanamume mwenzake nusu milioni jamaa zake wakishuhudia baada ya kufumaniwa akipapasa mke wa mwenyewe.

Mume wa mwanadada alikuwa amepashwa kuhusu vituko vya buda na akaamua kumkomesha.

“Mke wako si mwaminifu. Kila uendapo safari ndefu, amezoea kualika mwanamume huku kwako. Chunguza na utaujua ukweli,” jirani alimdokezea.

Jamaa alikuwa dereva wa malori yaliyosafirisha bidhaa kutoka Mombasa hadi Kigali.

Habari hizo zilikuwa sawa na nyundo iliyomteremkia utosini.

Alijiunga na wanaume wenzake katika baa jioni hiyo kujaribu kuyafukuza mawazo mazito yaliyomkosesha furaha. Ni huko katika baa alikozinduliwa na kuelezwa namna ya kufanya.

“Patafuka moshi kisha palipuke moto! Kuna mtu atakayeumia,” jamaa alisema.

Asubuhi ya siku iliyofuata, aliagana na mkewe akamwambia anafunga safari ndefu ya kuvuka mpaka hadi nchini DRC.

Alipoondoka, badala ya kuenda mbali, alifika nyumbani kwa rafikiye. Alikaa huko kwa siku nne na siku ya tano, jirani alimpigia simu.

“Mchovya asali ashafika tayari. Usikawie. Njoo mara moja utawakuta,” jirani alimpasha kwa simu.

Moyo ulimdunda kadri alivyopiga hatua kukaribia kufika kwake.

Alipobisha, mkewe alikataa kufungua.

“Fungua hapa mara moja! Mimi ni mumeo nimerudi,” jamaa alipaza sauti.

“Uongo! Uongo! Mume wangu kanambia amesafiri kuelekea nchi jirani. Wewe ni mwongo,” mke alisisitiza.

“Mumeo aliyekwambia atafunga safari aligundua unamla kivuli na amerudi. Usipofungua, nauvunja mlango na kumwaga damu,” jamaa aling’aka kwa hasira.

Mama yake ndiye alifika kumtuliza. Jamaa za mchovya asali waliitwa naye jamaa akasema bila nusu milioni angeua mtu.

Ilibidi alipwe pesa hizo ndipo alipoutupa upanga na kisu chini.

Mchovya asali alipitishwa mlango wa nyuma huku aibu ikimfunika kama blanketi akiafiki methali isemayo: Siku za mwizi ni arubaini.

You can share this post!

TAHARIRI: Ukora katika kusajili wapigakura uzuiwe

Idadi ndogo ya wanaojiandikisha wawe wapigakura yashuhudiwa...