Dondoo

Buda aonya polo kuhusu ulafi wa binti

December 14th, 2020 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KAVISUNI, KITUI

MZEE mmoja wa hapa, alizua purukushani nyumbani kwake akidai binti yake alikubali kuolewa na mpenzi wake kwa sababu ya pesa za jamaa!

Inasemekana demu alimpeleka mpenziye kumtambulisha kwa wazazi wake lakini mzee akamuonya kuhusu binti yake.

“Umefanya vizuri kuja hapa kwangu lakini nataka utahadhari sana na binti yangu. Usidhani anakupenda kwa dhati, anakupenda kwa sababu una mali tu. Kwa hivyo kuwa mwangalifu kwa kuwa anaweza kukuacha wakati wowote ukiwa umefilisika,” mzee alimwambia polo.

Inasemekana jamaa alipigwa na butwaa na kutilia maanani maneno ya mzee huyo. Hata hivyo, kwa upande wake demu alikasirikia baba yake na kumlaumu vikali.

“Baba, kwa nini unaniaibisha mbele ya watu? Mbona mama yangu hajalalamika na kuniharibia sifa? Mimi sina tamaa ya mali wala pesa. Wakati nimepata mume mwenye uwezo wa kunilipia mahari unaniharibia mipango yangu, umeniudhi sana,” demu alimwambia babake kwa hasira.

Licha ya demu kulalamika, mzee alisimama kidete na kushikilia msimamo wake.

“Mimi sipendi kudanganya. Wewe ni binti yangu na ninakujua vizuri. Umekuwa na wanaume wangapi na hao wote ulipowaacha kila mmoja alikuwa akilalamika kuwa una tamaa ya pesa na unapenda anasa kupindukia,” mzee aliongeza.

Polo alizidi kuingiwa na baridi mzee alipoendelea kuanika tabia za binti yake.

“Mimi siwezi kukubali mahari kutoka kwa mwanamume hivi hivi. Lazima niseme ukweli kwa sababu ninajua ndoa sio kitu cha kuchezea jinsi unavyofikiri,” mzee alimweleza binti yake.

Duru zinasema jamaa alimweleza demu asirushiane maneno na baba yake. Jamaa alimshukuru mzee kwa ushauri wake na akamhakikishia demu kuwa atafanya uamuzi huru kuhusu uhusiano wao.