Dondoo

Buda aoza bintize kulipia deni

February 15th, 2020 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KAMANDIO, KITUI

MZEE wa hapa alishangaza wakazi kwa kumtaka mwenzake ampe wasichana wake wawili ili waolewe na wavulana wake kama njia ya kumlipa deni.

Inasemekana aliyedaiwa alikubali takwa hilo lakini wasichana wake walikataa kabisa kuolewa bila hiari yao. Duru zinasema kwa miaka mingi, mzee alikuwa akimdai mwenzake mbuzi kumi lakini hakuonyesha dalili za kulipa.

Siku ya kioja, alienda kudai deni lake na wakazozana kwa muda akitisha kuchukua hatua za kisheria. Baada ya kugombana kwa muda, aligundua mwenzake hakuwa na uwezo wa kumlipa na akadai kwamba alikuwa na suluhisho.

“Nakudai mbuzi 10 lakini hujawahi kuniletea hata mmoja. Kama umeshindwa kunilipa nina njia murwa ya kunilipa deni langu,” mzee alisema.

Mzee alimtaka mwenzake akubali wavulana wake ambao tayari walikuwa wamekomaa waoe wasichana wake wawili.

“Una wasichana na mimi nina wavulana pekee. Wavulana wangu wanatafuta wasichana wa kuwaoa lakini ningependekeza waoe wasichana hawa wako warembo ili wanizalie wajukuu,” mzee alimwambia mwenzake.

Inasemekama mzee alijikuna kichwa lakini kwa sababu hakuwa na namna nyingine ya kumlipa mwenzake, alikubali ila alimsihi mwenzake ampe muda afanye mazunguzo na binti zake. Hata hivyo, wasichana hao walikataa katakata na kumlaumu baba yao kwa kuwaoza bila hiari yao. Mama yao aliungana nao kumlaumu mumewe kwa kutaka kubadilisha binti zake na deni.

“Hapo hautoboi hata, hatuwezi kukubali pendekezo lako na mzee mwenzako. Tutakachofanya ni kukusaidia kulipa deni lakini kuolewa, sahau,” mmoja wao alimweleza.