Dondoo

Buda avuruga harusi ya binti akidai mahari

February 4th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

KARATINA, NYERI

HAFLA moja ya harusi mtaani hapa ilisimamishwa kwa muda baba ya kipusa alipozua balaa akitaka kulipwa mahari.

Penyenye zinasema mzee alidai hakuwa amempa binti yake baraka za kuolewa. Alimlaumu mkewe kwa kushirikiana na familia ya Bw harusi kutumia njia za mkato.

Kulingana na mdokezi mzee huyo ni mraibu wa mvinyo na wakati wa maandalizi ya harusi hakuwa akipatikana.

Duru zinasema kwa kawaida huwa anafika kwake usiku wa manane na kuamka kwenda kwa mama pima alfajiri na mapema. Licha ya mke wake kumfahamisha kuhusu harusi ya binti yao, hakushughulika.

Siku ya sinema, ambayo binti yake na mpenzi wake walikuwa wakifunga pingu za maisha, jamaa alirauka na kuelekea kwa mama pima ilivyokuwa kawaida yake. Kanisani,harusi ilianza na maharusi wakavishana pete bila tatizo.

Wakati wa kusherehekea mlo ndipo jamaa alifika akiandamana na kundi la wazee wakiwa walevi.”Sikuruhusu binti yangu aolewe kwa sababu sijapata mahari. Ndio maana sijakuwa nikihudhuria mipango ya kuandaa harusi,” aliwaka mzee akionekana kuzidiwa na makali ya mvinyo.

Karamu ilivurugwa wazee hao wakitaka baba ya kidosho alipwe mahari mara moja. “Kaisari apewe kilicho chake, huyu mzee msipomlipa mahari huyu msichana hamtaenda naye,” wazee hao waliambia familia ya bw harusi.

Inasemekana binti yake alitokwa na machozi. Juhudi za pasta na wazee wa kijiji kutuliza kundi hilo ziligonga mwamba, wakitishia kulaani waliokaidi amri yao.

Kikao cha dharura kiliitwa na haijulikani kilichoafikiwa, kwani wazee hao baadaye waliondoka na kuenda zao bila kusema chochote.