Dondoo

Buda mlevi achoma mtoto kwa uji moto

October 30th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

Kiima Kimwe, Machakos

JOMBI wa hapa alisukumwa seli baada ya kumchoma mwanawe kwa uji moto akiwa mlevi. Inasemekana kuwa ni mkewe aliyeripoti kwa polisi baada ya kisa hicho cha asubuhi. Kulingana na mdokezi, jamaa alifika kwake asubuhi akiwa mlevi chakari na kuanza kugombana na mkewe.

Mkewe alitoka chumba cha kulala na kuelekea jikoni ambapo watoto walikuwa wakitayarisha uji na jamaa akamfuata akiendelea kumgombeza.

“Jamaa alifika nyumbani akiwa mlevi. Ilikuwa asubuhi na mkewe hakufurahishwa na tabia yake. Alipomuuliza kwa nini alikesha akilewa jamaa alipandwa na hasira na kuanza kuzusha.

Alimfuata mkewe jikoni ambapo watoto walikuwa wakiandaa uji na kuendelea kuvurugana na mkewe,” alisema mdokezi.

Ni katika kizaazaa hicho ambapo jamaa aliteleza na kuangusha sufuria ya uji uliomchoma mwanawe mguuni.

“Mkewe kuona mwanawe amechomeka, alikasirika. Alimpatia huduma ya kwanza kisha akaelekea kituo kidogo cha polisi kilichokuwa karibu kupiga ripoti huku jamaa akiweweseka hadi chumba cha kulala na kujilaza kitandani,” alisema mdokezi.

Baada ya kupiga ripoti kwa polisi, mkewe alimpeleka mwanawe hospitali huku jamaa akiendelea kung’orota kitandani. Kulingana na mdokezi, madaktari walimweleza kwamba mtoto huyo alikuwa na majeraha mabaya sana na aliyeyasababisha alifaa kuchukuliwa hatua.

“Hata kabla ya mkewe kuondoka hospitali, polisi walienda na kumkamata jamaa huyo na kumpeleka kituoni. Jamaa alikubali kwamba alikuwa amesababisha vurugu ambapo uji ulimwagika na kumchoma mwanawe mguuni lakini akasema hakufanya hivyo makusudi,” alieleza mdokezi.

Taarifa yake kwa polisi iliwiana na ya mtoto na mama yake. Jamaa aliomba msamaha na akaachiliwa akionywa kuwa atachukuliwa hatua akirudia makosa.