Dondoo

Buda taabani kufanyia yaya karamu ya bethidei

April 18th, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI,

MURANG’A MJINI

KIZAAZAA kilishuhudiwa katika boma moja mjini hapa mtu na mkewe walipofokeana jamaa alipomwandalia yaya karamu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa na kumnunulia zawadi.

Inasemekana kijakazi aliandaliwa sherehe ya kufana na mume wa mdosi wake hali iliyofanya wawili hao kuanza kuzozana.

“Mke wa polo alianza kuonea kijakazi gere mumewe alipogharamia sherehe ya mwanadada huyo. Mbali na kuandaa sherehe hiyo polo alimnunulia kijakazi mavazi ya kupendeza pamoja na simu mpya,” alisema mdaku wetu.

Yasemekana mke wa polo alianza kulalamika na kushuku kwamba huenda wawili hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi. “Kwa nini unaandalia kijakazi sherehe kubwa hapa nyumbani kwangu.

“Tangu unioe haujawahi kuandaa sherehe yeyote ya kukumbuka umbali tuliotoka lakini leo umeamua kunitia machungu kwa kuandalia kijakazi huyu mchafu sherehe kubwa kiasi hiki. Una uhusiano gani na yeye?

“Nashuku umeanza kunitema na kuanza kula za haramu na kijakazi huyu. Umemnunulia mavazi na simu ya bei ghali.

“Hakuna sherehe itakayofanyika hapa,” mkewe polo alisema. Licha ya mke wa polo kulalamikia, kalameni alimjibu kwa ukali.

“Wewe ni mwanamke sampuli gani. Kuna shida gani ya kuandalia kijakazi sherehe kubwa? Una fikira mbaya.

“Tunapaswa kuonyesha kijakazi mapenzi kwa mchango wake kwa familia lakini unanifokea,” polo alisema.

Hata hivyo mkewe alisisitiza kuwa sherehe haingefanyika kwake na akaapa kumchukulia mumewe hatua akijaribu kumtema kwa sababu ya kijakazi huyo.

Kijakazi alisisitiza hakuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi na mzee wa boma. Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya kioja hicho.

…WAZO BONZO…