Kimataifa

Buhari aanza kufunga shule za Kiislamu zilizogeuka ‘jela’

October 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LAGOS, NIGERIA

RAIS wa Nigeria, Muhammadu Bahari ameagiza msako mkali dhidi ya shule za Kiislamu baada ya polisi kugundua kuwa zinatumiwa kama jela kuwadhulumu wanaume na wavulana kwa kuwapiga na kuwafunga kwa minyororo kama watumwa.

Buhari alichukua hatua hiyo baada ya polisi kuvamia shule moja eneo la Daura, Katsona, mji wa kwake nyumbani na kuwaokoa watu 300 waliokuwa wamefungiwa humo.

Polisi walisema kwamba waligundua watu hao walikuwa wakidhulumiwa kama watumwa huku haki zao zikikiukwa. Waliwaokoa wanafunzi hao katika msako wa pili uliolenga shule za Kiislamu.

Mwezi jana, polisi walipata mamia ya wanafunzi katika mazingira sawa kwenye shule moja iliyoko jimbo jirani la Kaduna.

“Bw Rais ameagiza polisi kuvunjilia mbali vituo hivyo na wote waliofungiwa ndani wakabidhiwe wazazi wao,” ilisema taarifa kutoka kwa msemaji wa rais.

“Serikali haiwezi kuruhusu vituo kama hivi ambapo watu, wanawake na wanaume wanateswa kwa jina la dini,” iliongeza taarifa hiyo.

Kabla ya polisi kuvamia shule hiyo wiki hii, mamia ya wafungwa walikuwa wametoroka, polisi walisema.

Polisi katika mji wa Katsina waliwaokoa watu 67 waliowapata wakiwa wamefungwa kwa minyororo na wengi wao walipelekwa hospitali kutibiwa, Superitenda wa polisi Isah Gambo aliambia maafisa wanahabari wa AFP.

“Nakwambia walikuwa katika hali mbaya tulipowapata,” alisema Gambo.

Mmoja wa waliookolewa aliambia wanahabari kwamba wakufunzi wao waliwapiga, kuwanajisi na hata kuwaua baadhi ya wanaume na wavulana waliofungiwa katika kituo hicho.

Alisema walikuwa na umri wa kati ya miaka saba na 40. Hata hivyo, madai hayo hayakuweza kuthibitishwa mara moja.

Ingawa kituo hicho kiliambia wazazi kuwa kiilikuwa kinatoa mafunzo ya kidini ya Kiislamu ili kuwasaidia kurekebisha watu wa familia zao waliopotoka, wakufunzi walikuwa wakiwatendea ukatili na kuwapokonya chakula au pesa walizotumiwa na jamaa zao.

Polisi walisema walimkamata mmiliki wa kituo hicho na walimu wawili na kwamba walikuwa wakiwasaka washukiwa wengine. Bw Gambo alisema watu 200 waliotoroka kituo hicho hawajulikani waliko. Afisa huyo alisema kwamba wanaendelea kuwaunganisha waliookolewa na familia zao.

“Wafungwa hao wanatoka sehemu tofauti za nchi -majimbo ya Kano, Taraba, Adamawa na Plateau,” alisema.

“Baadhi yao si raia wa Nigeria. Wanatoka Niger, Chad na hata Burkina Faso na nchi nyingine.”

Shule zinazotoa mafunzo ya Kiislamu zinazofahamika kama Almajiris, zinapatikana kwa wingi kaskazini ya Nigeria.

Shirika la Muslim Rights Concern, linalohudumu eneo hilo linakadiria kuwa watoto milioni 10 huwa wanahudhuria shule hizo.

Buhari alisema serikali inapanga kupiga marufuku shule hizo lakini hakueleza chochote kuhusu shule ya Katsina.