Michezo

Bundes FC yazima makali ya Gogo Boys na kubeba taji la Slums Champion

October 23rd, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

LICHA ya tishio la mlipuko wa virusi vya corona uliochangia shughuli za michezo kusitishwa, vijana wengi wanazidi kutifua vumbi kwenye mechi za kuwania mataji na kupimana nguvu.

Timu ya Bundes FC imebeba taji la Slums Champion baada ya kutifua vumbi kali na kuzima makali ya Gogo Boys.

Mashindano hayo yaliyojumuisha takribani timu 14 za wanaume yaliandaliwa na kudhaminiwa na Yakub Jaffar.

HAT-TRICK

Wapiga gozi wa kikosi hicho chenye makao yake katika mtaa wa Dagoretti walionyesha wenzao wa Gogo Boys jinsi ya kusakata gozi walipowaliza mabao 4-1 katika fainali Uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Tony Nyangeso alipiga ‘hat trick’ huku Brian Musee akitikisa nyavu mara moja. Bao la kufutia machozi la Gogo Boys ya kocha, Wilberforce Chisira ambayo hushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili lilifunikwa kimiani na mfumaji matata Hillary Shirao.

Patashika hiyo ilianza kwa kasi huku vijana wa Bundes FC ambao hushiriki mechi za kufukuzia mataji na kirafiki tangu kikosi hicho kianzishwe mwaka 2015 kufunga bao la kwanza kunako dakika ya kumi kupitia Tony Nyangeso kabla ya Shirao kusawazishia Gogo Boys dakika tano baadaye.

Waamuzi wakiongea na manahodha wa Gogo Boys na Bundes FC. Picha/ John Kimwere

KJ SUPER CUP

”Tunashukuru wachezaji wetu kwa kutimiza azma yetu kunyamazisha Gogo Boys ambayo ni kati ya klabu mahiri katika mtaa wa Kibera,” kocha wa Bundes, Bill Okumu alisema.

Bundes FC ambayo hujumuisha wachezaji kutoka mtaa huo inajivunia kushinda mataji mbali mbali tangu ibuniwe. ”Siwezi kukumbuka mataji ya mataji ambayo tumebeba lakini ninachofahamu kwamba tumeshinda zaidi ya tano ikiwamo KJ Super Cup na SportPesa Tournament,” kocha wa Bundes alisema na kuongeza kuwa wamepania kutetea taji hilo kwenye makala ya pili ya Slum Champion mwezi Desemba 2020.

Kocha huyo alitoa pongezi za dhati kwa wachezaji aliotaja kuwa waliibeba wenzao pakubwa ili kutwaa ufanisi huo. Alitaja wanasoka hao kama Hillary Okoth (nahodha), Eric Mungai, Peter Njuguna, Joseph Mutinde na December Kisaka.

MWATT FC

Kwenye nusu fainali, Bundes FC ilitandika Korogocho Youth mabao 5-3 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare tasa. Nayo Gogo Boys ilinasa tiketi ya fainali baada ya kuandikisha ufanisi wa mabao 3-2 dhidi ya RiftValley Soccer Academy (RVSA). Katika fainali ya Kanda ya Dagoretti Bundes ililaza Mwatt FC 3-1, Kanda ya Rongai, RVSA ilikomoa Cush FC 3-1 huku Korogocho Youth ikizima Vision FC 2-1 katika Kanda ya Kariobangi.