Michezo

BUNDESLIGA 2: Dynamo Dresden yaweka kikosi kizima karantini

May 10th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KLABU ya Dynamo Dresden inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Ujerumani (Bundesliga 2) imeweka kikosi chote na benchi nzima ya kiufundi katika karantini kwa kipindi cha wiki mbili baada ya wachezaji wawili wa kupatikana na virusi vya corona kambini.

Hatua hiyo huenda sasa ikatatiza juhudi za kurejelewa kwa kampeni zilizosalia katika soka ya Ujerumani msimu huu.

Vinara wa Bundesliga na Bundesliga 2 wamekuwa wakijitahidi kufanikisha mipango ya kukamilisha vipute hivyo msimu huu kuanzia Jumamosi ya Mei 16, 2020.

Kufaulu kwa hilo kutafanya Bundesliga kuwa ligi ya kwanza kurejelewa kati ya zote barani Ulaya licha ya kwamba virusi vya corona havijadhibitiwa vilivyo duniani kote.

“Ukweli ni kwamba hatuwezi kufanya mazoezi wala kushiriki mchuano wowote katika kipindi cha siku 14 zijazo,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Dynamo.

Mnamo Mei 7, 2020, Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) lilisema kwamba kampeni za ligi za soka nchini humo zitarejelewa chini ya mwongozo wa kanuni kali zaidi za afya huku michuano yote ikisakatiwa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki.

Wachezaji wa vikosi vyote watatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya ambavyo vitaendelezwa mara kwa mara katika sehemu ya makazi ya kila kikosi.

Kwa mujibu wa waendeshaji wa kipute cha Bundesliga, takriban watu 300 pekee wakiwemo wachezaji, maafisa wa usalama na wafanyakazi wa klabu zinazoshiriki mechi kwa wakati mmoja ndio watakaoruhusiwa ugani siku ya gozi.

Kivumbi cha Bundesliga kiliahirishwa kwa muda usiojulikana mnamo Machi 13, 2020.

Wanasoka wa takriban vikosi vyote vya Bundesliga walirejea kambini mnamo Aprili 15 na wamekuwa wakishiriki mazoezi katika makundi.

Kwa mujibu wa Ralf Minge ambaye ni meneja wa timu ya Dynamo inayovuta mkia kwenye jedwali la Bundesliga 2, itakuwa vigumu kwa kikosi chao kukamilisha kampeni za msimu huu na wametaka maafisa wa afya na waendeshaji wa soka ya Ujerumani (DFL) kuingilia kati na kutafutia hali yao ya sasa suluhu.

Dresden walitarajiwa kuanza upya kampeni za soka ya Ujerumani mnamo Mei 17 katika gozi dhidi ya Hannover 96 ugani HDI Arena.