Bunduki 22, risasi 500 zapatikana katika nyumba mtaani Kilimani

Bunduki 22, risasi 500 zapatikana katika nyumba mtaani Kilimani

NA MARY WAMBUI

KUPATIKANA kwa bunduki 22 na zaidi ya risasi 500 katika afisi za Wycliffe Lugwili mtaani Kilimani, Nairobi, Jumatano, kumefichua jinsi ambavyo waliokuwa wamiliki bunduki hushiriki biashara haramu baada ya leseni zao kufutiliwa mbali.

Bunduki hizo zilipatikana wakati maafisa walikuwa wakitoa ulinzi kwa madalali kutokana na deni la Sh4 milioni ambalo ni kodi ya nyumba ya miaka miwili ambayo mmiliki wa nyumba hiyo hajalipwa.

Stakabadhi ambazo Taifa Leo ilizilipata zilionyesha kuwa, Lugwili hakuwa amelipa kodi ambayo kila mwezi ni Sh173,000.

Pia, ilibainika kuwa Lugwili alifahamu vyema mpango wa kupiga mnada mali yake lakini hakupinga na alijiwasilisha katika kituo cha polisi cha Kilimani pamoja na mawakili wake baada ya silaha hizo kupatikana afisini mwake jana Jumatano.

Baadaye, alichukuliwa na makachero ambao walimkabidhi kwa Polisi wa Kupambana na Ugaidi (ATPU) wanaoendelea kumchunguza.

Lugwili alipokezwa leseni ya kumiliki bunduki hadi Agosti 3, 2019 wakati Bodi ya kutoa Leseni ya Kumiliki Bunduki ilipoharamisha leseni yake ikishuku biashara alizokuwa akifanya.

Mnamo Agosti 3, 2019, Mwenyekiti wa bodi hiyo Charles Mukindia alitaja uchunguzi unaoendelea dhidi ya Lugwili kama sababu ya kuondoa leseni yake.

Bw Mukindia, alieleza Taifa Leo, kuwa bunduki zilizopatikana katika afisi ya Lugwili ni zile ambazo wafanyabiashara nchini wameruhusiwa kuuza.

  • Tags

You can share this post!

Hakuna ufadhili kwa mashirikisho ya michezo, wizara yasema...

Wajackoyah atikisa wagombea wakuu

T L