Habari za Kitaifa

Bunduki mali ya Uganda yaaminika iko Kenya

February 1st, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

HUENDA majambazi wenye maficho katika Kaunti ya Kisumu ndio waliomshambulia kimabavu polisi wa Uganda ndani ya taifa lake na kumpokonya bunduki aina ya AK47, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imesema.

DCI ilisema polisi huyo alikuwa anahudumu katika kituo cha polisi cha Central kilichoko mjini Tororo.

Idara hiyo ilisema katika taarifa rasmi ya Januari 31, 2024, kwamba uamuzi huo uliafikiwa baada ya tukio moja lililotokea polisi wakipiga doria eneo la Nyalenda, Kisumu.

Kwa mujibu wa DCI, maafisa hao walikumbana na washukiwa wakiwa wamejihami kwa bunduki mbili, moja ikiwa na ishara za kuwa ile ya serikali ya Uganda.

Bunduki hiyo ilifichuliwa kuwa na usajili wa UG POL 861314 09446.

“Maafisa wa eneo la Kasagam katika Kaunti ya Kisumu walikuwa katika doria eneo la Nyalenda na wakakumbana na gari aina ya Toyota Axio lenye nambari za usajili KDL 301P likiwa na wanaume watano ndani,” taarifa ya DCI ikasema.

Waliposimamishwa na maafisa hao, wanaume hao walifungua milango na wakatimua mbio.

Polisi waliita makachero kuchunguza gari hilo na ndipo bunduki hiyo ya Uganda ikagunduliwa ikiwa na nyingine za watu kujitengenezea nyumbani.

Ripoti hiyo inasema kwamba kwa sasa mikakati imewekwa ya kusaka washukiwa hao huku gari lao likiwa mikononi mwa polisi kwa sasa.

[email protected]