Habari

Bunge kupitisha miswada 13 kuiandalia njia ripoti ya BBI

November 4th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa limeratibu miswada 13 linalolenga kupitisha kufanikisha utekelezaji na utekelezwaji wa mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Uongozi wa bunge hilo utakutana wiki hii kuamua idadi ya miswada ambayo itawasilishwa bungeni kama miswada huria na ile ambayo itashughulikiwa kama sehemu ya miswada ya marekebisho ya sheria mbalimbali (Miscellaneous amendments bills).

Maafisa wa bunge tayari wameagizwa kuandaa miswada husika kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kwa mijadala kuanzia mwezi huu wa Novemba. Bunge lilirejelea vikao vyake Jumanne baada ya kukamilika kwa likizo fupi.

Kiranja wa walio wachache Junet Mohamed alithibitisha kuwa miswada hiyo 13 itashughulikiwa kwa haraka na kupitishwa ili kutoa nafasi kufanyika kwa kura ya maamuzi “kabla ya Juni mwaka wa 2021.”

“Tumejipanga na tuko tayari kufikia maamuzi yatakayofanikisha kupitishwa kwa miswada hiyo wezeshi haraka iwezekanavyo,” akasema Bw Mohamed ambaye ni mbunge wa Suna Mashariki.

Baadhi ya miswada ambayo imeratibiwa kujadiliwa na kupitishwa ni Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Bodi ya kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (HELB) inayodhaminiwa na Mbunge Maalum Gideon Keter.

Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Tume ya Huduma za Bunge (Judicial Service Bill) iliyoko mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC), Mswada wa Kura ya Maamuzi na Mswada wa kubuni Hazina ya Maendeleo ya Wadi uliodhaminiwa na Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata.

Marekebisho ya Sheria ya HELB kwa mfano yanalenga kuhakikisha kuwa walionufaika kwa mkopo huo utaanza kulipwa wakati ambapo mhitimu atapaka ajira. Pia unapendekeza kuwa waliofaidi na mkopo waanze kulipa baada ya miaka minne, baada ya kupata ajira.