Habari Mseto

Bunge kuzindua kanuni zake katika Kiswahili leo

November 12th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa linatarajiwa kupiga hatua muhimu katika matumizi ya lugha ya Kiswahili kuendeshea shughuli zake kwa kuzindua kanuni za bunge zilizotafsiriwa kwa lugha hiyo, leo.

Hafla ya uzinduzi imepangiwa kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya Hotuba yake kuhusu Hali ya Taifa mbele ya kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa na Seneti.

Itakuwa mara ya kwanza kwa wabunge kuanza kutumia kanuni ziliandikwa kwa Kiswahili japo baadhi yao wamekuwa wakichangia mijadala kwa lugha hii kwani ni mojawapo ya lugha rasmi bungeni, kulingana na kipengele cha 120 cha Katiba ya Kenya.

Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai alisema uzinduzi huo ni kilele cha shughuli ya utafisiri, na usanifishahi wa kanuni hizo, iliyoendeshwa na jopo kazi maalum kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

Jopokazi hilo lilisaidiana na maprofesa wa Kiswahili kutoka vyuo vikuu vya Kenya na wataalamu wa lugha hii kutoka Kenya na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA).

“Ama kwa hakika Alhamisi ni siku muhimu zaidi katika historia ya bunge la kitaifa kwani kwa mara ya kwanza wabunge wataanza kutumia nakala za Kanuni za Kudumu zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Hii imetuweka katika kiwango kimoja na bunge la taifa jirani la Tanzania ambalo kanuni zake na machapisho mengine yanapatikana kwa lugha ya Kiswahili,” alinukuliwa akisema.

Mchakato wa kutafsiri kanuni za Seneta kwa Kiswahili pia umeanza na unatarajiwa kukamilika mapema mwaka ujao.Afisa wa bunge ambaye ni mwanachama wa jopokazi lililooendesha kazi ya hiyo ya utafsiri jana aliambia Taifa Leo kwamba mradi huo ni sehemu mpango mpana wa asasi ya bunge kuandaa sajili rasmi ya bunge; lugha ya mahsusi itakuwa ikitumika na wabunge kuandaa hoja na miswada na kushiriki mijadala.

“Hatimaye wabunge wataweza kutunga hoja, miswada, maswali na hata ripoti zao kwa lugha ya Kiswahili inayozingatia sajili ya bunge. Ni sajili hiyo ilizingatiwa katika utafsiri wa Kanuni za Kudumu ambayo nakala zake zitazinduliwa na Rais Alhamisi. Hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya Kiswahili nchini,” akasema afisa huyo ambaye aliomba tusimtaje jina.

Kama hatua ya kuendeleza matumizi ya Kiswahili bungeni, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amependekeza kuwa kikao cha Alhamisi alasiri kiwe kikiendeshwa mhasusi kwa lugha ya Kiswahili, pendekezo ambalo litaanza kutekeleza “hivi karibuni.”

Isitoshe, asasi ya bunge inapanga kuanzisha idara mahsusi ya Kiswahili itakayoshirikisha masuala yote ya matumizi ya lugha hii kuendeshea shughuli za mabunge yote mawili.Miongoni mwa wabunge ambao huchangia hoja na mijadala kwa lugha ya Kiswahili ni Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, Mishi Mboko (Likoni), Badi Twalib Jomvu, Andrew Mwadime (Mwatate).

Katika Seneti wale ambao hutumia Kiswahili katika mijadala ukumbini ni maseneta Isaac Mwaura (seneta maalum), Stewart Madzayo (Kilifi), Mohamed Faki (Mombasa) na Issa Juma Boy (Kwale).

Isitoshe, Bw Mwaura, ambaye pia ni mmoja wa wasaidizi wa Spika wa Seneti Kenneth Lusaka amepiga hatua, kimakusudi, kwa kuendesha vikao vya kwa lugha ya Kiswahili nyakati za zamu yake ya kuhudumu kama Spika wa Muda.

Katika mahojiano na Taifa Leo juzi Mwaura alisema kuwa Wakenya wamechangamkia hatua yake ya kuongoza vikao vya seneti kwa lugha ya Kiswahi.

“Hata Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alinieleza kuwa alipendezwa sana na hatua yangu ya kuongoza vikao vya juzi vya vya kujadiliwa na kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Fedha Baina ya Kaunti (CARA) ya 2020. Hii ni kwa sababu katika historia ya taifa hili hakuna Spika ambaye amewahi kuongoza vikao vya bunge kwa lugha ya Kiswahili licha ya kwamba Kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi bungeni,” akaongeza.