Bunge la Kaunti ya Kiambu kujadili ripoti ya BBI

Bunge la Kaunti ya Kiambu kujadili ripoti ya BBI

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu inajiandaa kujadili mswada wa ripoti ya BBI ili kuupitisha iwapo utapata uungwaji mkono katika bunge la kaunti.

Gavana wa kaunti hiyo James Nyoro alisema tayari wamekubaliana na madiwani kuwa watapitisha ripoti hiyo ili kuweka mfano kwa kaunti nyinginezo za Mlima Kenya.

Tayari Kaunti ya Siaya ilipitisha BBI na madiwani wako tayari kutoa hamasisho kwa wananchi.

Bw Nyoro alisema viongozi wanastahili kusema ukweli wa mambo kuhusu ripoti hiyo badala ya kueneza propaganda.

“Tunajua kuna viongozi wachache ambao hawataki ripoti hiyo ipite lakini hatutakubali wananchi waendelee kuyumbishwa kuhusu ripoti hiyo,” alisema Bw Nyoro.

Alisema ripoti hiyo inaipa kaunti ya Kiambu nafasi kubwa ya kimaendeleo kwa sababu kuna maeneobunge sita mapya ambayo yatapatikana.

Baadhi ya maeneo hayo ni Thika Mashariki na Magharibi, Juja, Ruiru, Kiambu na Kabete.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jana alipizuru eneo la Makutano Kilimambogo, kukagua mradi wa ujenzi wa barabara.

Alieleza kuwa ripoti hiyo itaongeza mgao wa fedha ambazo zinatumwa na serikali kutoka asilimia 15 hadi 35.

Alisema rekodi ya Rais Uhuru Kenyatta katika maendeleo kote nchini inajieleza yenyewe ambapo kama ni barabara, umeme, na maji yanapatikana katika maeneo mengi ya nchi.

Hata hivyo, wakosoaji wa BBI bado wanaendelea kuutaja ubaya wa ripoti hiyo wakidai mwananchi hajapewa muda wa kutosha kuichambua na kuielewa.

“Kila kiongozi ifikapo 2022 atalazimika kueleza wananchi ni kipi aliwafanyia cha maana. Kwa hivyo siasa za chuki hazitapata nafasi wakati huo,” alisema Bw Nyoro.

Alihimiza kaunti zingine zifanye hima kuona ya kwamba zinapitisha ripoti hiyo kwa sababu “ina manufaa makubwa kwa mwananchi.”

Aliwashauri viongozi wasipande chuki kwa wananchi kwa sababu ya ripoti ya BBI bali wawe mstari wa mbele kusema ukweli wa mambo.

“Huu sio wakati wa kuchochea wananchi kwani tumesalia na miezi 18 kuelekea uchaguzi. Tusiweke akili zetu kwa uchaguzi kwa wakati huu bali tuzingatie ajenda muhimu za serikali ili mwananchi apate maendeleo,” alisema Bw Nyoro.

  • Tags

You can share this post!

Manchester City waponda Liverpool na kujiweka pazuri kutwaa...

UDAKU: Boateng achepukiwa sawa tu na afanyavyo!