Habari Mseto

Bunge la Lamu lapitisha mswada wa Bajeti ya Muda ya Sh3 bilioni

March 2nd, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

BUNGE la Kaunti ya Lamu limepitisha kwa pamoja mswada wa Bajeti ya Muda ya Sh 3 bilioni, hivyo kuiwezesha serikali ya kaunti hiyo kutumia kima cha fedha hizo katika mwaka wa kifedha unaokamilika kufikia Juni 30, 2018.

Katika bajeti hiyo, Idara ya Ardhi na Mipangilio ya Miji ilitengewa mgao wa juu zaidi wa Sh 206 milioni huku Idara ya Aya ikitengewa Sh 174 milioni.

Idara ya Mawasiliano na Masuala ya Utawala kiutandawazi ndiyo iliyotengewa mgao wa chini zaidi wa Sh 11 milioni ilhali sekta ya Utalii pia ikitengewa mgao wa chini wa Sh 24 milioni pekee.

Katika bajeti hiyo, Idara ya Elimu, Michezo, Vijana na jinsia ilipata Sh 83 milioni, uvuvi na mifugo ikatengewa Sh 60 milioni ilhali ile ya Kilimo na Unyunyizaji maji ikitengewa Sh 58 milioni.

Mswada huo ulipitishwa bila marekebisho yoyote katika kikao cha bunge kilichoongozwa na Spika, Abdul Kassim Ahmed.

Madiwani wa kaunti ya Lamu wakiwa bungeni. Walipitisha mswada wa bajeti ya muda ya Sh3 bilioni. Picha/ Kalume Kazungu

Akizungumza na wanahabari nje ya majengo ya Bunge muda mfupi baada ya kupitisha mswada huo, Naibu Spika, Bw Abdalla Baabad, ambaye pia ni Mwakilishi wa Wadi ya Kiunga, alisema waliafikia kupitisha bajeti hiyo ya muda ili kuwezesha kuendelezwa kwa miradi mbalimbali eneo hilo.

Alisema fedha nyingi zaidi zilielekezwa katika idara ya ardhi ikizingatiwa kuwa sekta hiyo iko na utata mwingi kagtika kaunti ya Lamu.

Bw Baabad pia alisema hawangeipa kipaumbele sekta ya utalii katika mgao wa fedha kutokana bna kwamba sekta hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto tele kutokana na usalama eneo hilo.

“Tuliweka fedha nyingi katika idara ya ardhi ili kusuluhisha matatizo chungu nzima yaliyoko kwenye sekta hiyo hapa Lamu. Japo sekta ya utalii ni uti wa mgongo wa Lamu, hatungetenga fedha nyingi kwa sekta hiyo mwaka huu kwani tumekuwa tukitumia fedha tayari katika kuutangaza utalii wa eneo hili,” akasema Bw Baabad.