Habari za Kitaifa

Bunge lahimiza TSC iwape ajira walimu wa JSS


MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti, Ndindi Nyoro, amehimiza Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuwapa ajira ya kudumu walimu wanagenzi wa Sekondari Msingi (JSS) mara tu bajeti itakapopitishwa.

Hii ni baada ya TSC kutengewa fedha za kuwaajiri walimu wote wanagenzi wa JSS kwa mikataba ya kudumu. Bw Nyoro vilevile alisema TSC imetengewa fedha za kutosha za kuajiri walimu wengine 20,000 ili kujaza pengo lililopo.

“Msicheleweshe kuwapa ajira ya kudumu walimu wanagenzi wa JSS hadi Januari mwaka ujao. Bajeti itakapopitishwa, mwaajiri walimu wa JSS,” alisema Bw Nyoro akipongeza bajeti kama inayotilia maanani watoaji huduma kwa raia.

Akizungumza Jumamosi katika eneo la Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale, kwenye hafla ya kuchangisha pesa, Mbunge huyo wa Kiharu alisema elimu ndicho kisawazishi cha pekee na kuwa serikali ina mikakati tosha ya kuimarisha sekta hiyo.

Sekta ya elimu imenyofoa kiasi kikubwa zaidi cha mgao wa bajeti ambapo imetengewa Sh656 bilioni.

Walimu wa JSS ambao wamekuwa kwenye mgomo tangu Aprili 17 na kuusitisha wiki iliyopita, Julai 5. Mahafala hao 46,000 walioajiriwa kama walimu wanagenzi 2019, walisema kusitishwa kwa mgomo wao ni wa kuipa TSC muda iwaajiri kwa mkataba wa kudumu.

Wanasubiri pia Bunge la Kitaifa lipitishe bajeti. Msemaji wao kitaifa, Omari Omari, alihimiza TSC kutoa notisi kuhusu kuthibitishwa kwa ajira yao bajeti itakapoidhinishwa.

“Tumetengea sekta ya elimu Sh658 bilioni kwa umuhimu wake. Mtu anayeishi Othaya, Pokot Magharibi na Lunga Lunga ni sharti watoshane kwa sababu ya elimu. Mtoto kutoka familia tajiri na anayetoka katika jamii maskini watasawazishwa na elimu,” alisema Bw Nyoro.

Alisema serikali vilevile imetengea sekta ya afya Sh3.7 bilioni ili kuwaajiri wahudumu wa afya wanagenzi kwa mikataba ya kudumu.

“Tunataka pia wapatiwe ajira ya kudumu,” alisema mbunge huyo.

Wakati huo huo, wabunge wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Bw Nyoro walimkashifu Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kueneza mfumo wa kugawa mapato kwa kuzingatia idadi ya watu almaarufu mtu mmoja, shilingi moja akionya kuwa utaeneza ukabila.

Badala yake, alimhimiza Naibu Rais kujishughulisha na masuala ya kuwaunganisha Wakenya na kuwezesha maendeleo nchini.

Mbunge wa Msambweni, Feisal Bader, alisema pendekezo la Naibu Rais litatenga hata zaidi baadhi ya maeneo.

“Maeneo yanayohitaji maendeleo yatazidi kutengwa kutokana na pendekezo hili. Barabara zetu mjini Kwale bado hazijawekwa lami kwa mfano Barabara ya Lunga Lunga-Kinango lakini ukienda kaunti kama vile Murang’a au Nyeri, barabara zote zimewekwa lami,” alisema Bw Bader.

Alimhimiza Naibu Rais kusitisha pendekezo hilo hadi barabara zote katika eneo la pwani zitakapowekwa lami huku akipigia debe usawa na haki.