Habari

Bunge laidhinisha hatua muhimu katika uteuzi wa msimamizi wa bajeti

December 4th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha na Mipango imeidhinisha uteuzi wa Bi Margaret Nyakango Nyang’ate kuwa Msimamizi wa Bajeti (CoB).

Kwenye ripoti ambayo iliwasilishwa bungeni Jumanne alasiri na mwenyekiti wa kamati hiyo Joseph Limo, inasema Dkt Nyang’ate amehitimu kimasomo na kitajriba kwa kazi hiyo.

“Baada ya kamati hii kumpiga msasa Margaret Nyang’ate aliyependekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kushikilia wadhifa wa Msimamizi wa Bajeti (CoB) kamati hii imeridhika kwamba amehitimu kwa kazi hiyo. Vilevile, wanachama walitosheka kwamba ana uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika masuala ya usimamizi wa fedha,” akasema Bw Limo alipowasilisha ripoti ya kamati yake.

Sasa ripoti hiyo itajadiliwa na kamati ya bunge lote mnamo Alhamisi alasiri ambapo inatarajiwa kuwa wabunge kuipitisha na kutoa nafasi kwa Rais Kenyatta kumteua rasmi Dkt Nyang’ate.

Baada ya kuteuliwa rasmi Dkt Nyang’ate ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Masuala ya Kifedha katika Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) atachukua mahala Agnes Odhiambo kwa miaka sita baada ya muda wake kukamilisha mnamo Agosti 17, 2019.

Kiti hicho sasa kiko wazi baada ya muda wa siku 90 ambao Rais Kenyatta alimteua Bw Stephen Masha kuhudu kukamilika mnamo Novemba 17, 2019.

Hii ndio maana Serikali za kaunti zimekuwa zikilalamika kwamba zimeshindwa kuwalipa wafanyakazi wao mishahara baada ya kukabiliwa na changamoto ya kuitisha pesa kupitia ofisi ya CoB.

Bw Masha ndiye alikuwa akitoa idhini kwa serikali za kaunti kutoa fedha kutoka akaunti zao katika Benki Kuu ya Kitaifa (CBK) kwa matumizi mbalimbali ikiwemo ulipaji wa mishahara.

Sasa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoB), Wycliffe Oparanya, anasema serikali za kaunti haziwezi kutoa fedha za matumizi kwa sababu hamna afisa wa kuzipatia idhini ya kufanya hivyo.

“Kutokana na hali hii, serikali za kaunti zimeshindwa kutoa malipo mbalimbali yakiwemo mishahara ya Novemba, fedha zinazostahili kulipa asasi za serikali, pesa za kununulia mahitaji ya kila siku na kugharimia malimbikizo ya madeni,” akasema Bw Oparanya ambaye ni Gavana wa Kakamega.

“Kwa hivyo, kaunti zote 47 hazijapokea mgao wao Sh31.6 bilioni wa mwezi wa Novemba, pesa ambazo zilifaa kutolewa mnamo Novemba 15,” akaongeza.

Kwa hivyo, Bw Oparanya aliitaka Serikali ya Kitaifa kuharakisha mchakato wa kujaza nafasi ya mshikilizi mpya wa ofisi ya msimamizi wa bajeti ili aweze kuidhinisha kutolewa kwa fedha za kaunti kufanikisha mipango ya utoaji huduma.

“Pia serikali inafaa kuwasilisha fedha zote ambazo zilifaa kuwa zimetolewa kufikia Novemba 15 ili kaunti ziweze kulipa madeni yao,” aliongeza.

Hatua ya kamati ya Bw Limo kuidhinisha jina la Dkt Nyang’ate sasa imeleta matumaini kwamba huenda wadhifa huo ujazwe wiki hii baada ya kamati ya bunge kupitisha ripoti hiyo.