Habari Mseto

Bunge laidhinisha Mutyambai kuwa Inspekta Jenerali mpya

April 3rd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumatano waliidhinisha uteuzi wa Hilary Nzoiki Mutyambai kwa wadhifa wa Inspekta Jenerali wa Huduma ya Polisi Nchini siku moja baadaya ya maseneta kukubali na uteuzi huo.

Bw Mutyambai sasa anatarajiwa kuapishwa wakati wowote kuanzia sasa kabla ya kuanza kazi ya kusimamia usalama wa kitaifa kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Wakijadili ripoti ya Kamati kuhusu Usalama wa Ndani na Utawala ambayo ilipendekeza uteuzi wa Bw Mutyambai kwa wadhifa huo, walimtaka apambane na ufisadi, haswa katika idara ya trafiki, mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na polisi, wizi wa mifugo, mashambulio ya kigaidi, ulanguzi wa dawa za kulevya, kuchipuza kwa magenge haramu, kati ya mauvo mengine.

“Tunajua anatosha kwa wadhifa huo, kutokana na tajriba ya miaka 27. Kibarua cha kwanza chafaa kuwa kukomesha mauaji ya kiholela yanatekelezwa na polisi katika maeneo ya Nairobi, Mombasa na Kaskazini Mashariki mwaka Kenya,” akasema kiongozi wa wengi Aden Duale.

Alisema wananchi hupotea katika hali ya utata na hatimaye miili yao inapatikana katika hifadhi za maiti.

Naibu kiongozi wa wachache bungeni, Bw John Mbadi alimtaka Bw Mutyambai azime kabisa mipango ya magaidi kutekeleza mashambulio nchini.

Nao wabunge Daniel Maanzo (Makueni), Dkt Robert Pukose (Endebess), Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) na Robert Mbui (Kathiani) walimtaka Bw Mutyambai kuwaadhibu vikali maafisa wa polisi wafisadi.

“Namtaka Bw Mutyambai kulenga zaidi idara ya trafiki ambako ufisadi umekita mizizi. Akomeshe kabisa huu mtindo wa barabara zetu kugeuzwa vituo vya kukusanya fedha,” akasema Bw Pukose.

Hadi alipopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa wadhifa huo Bw Mutyambai alihudumu kama Naibu Mkurugenzi wa idara inayosimamia mapambano dhidi ya ugaidi katika NIS.

Anachukua mahala pa Inspekta Jeneral wa Polisi anayeondoka Bw Joseph Boinnet ambaye aliteuliwa na Rais Kenyatta kuwa Naibu Waziri wa Utalii na Huduma za Wanyama Pori.