Bunge lajadili kwa uzito changamoto ya uhaba wa mafuta

Bunge lajadili kwa uzito changamoto ya uhaba wa mafuta

NA CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa limeanzisha uchunguzi kuhusu jumla ya pesa ambazo serikali ilikusanya kuelekezwa kwa Hazina ya Mafuta kuanzia Septemba 2021 huku wabunge wakitenga muda kujadili kero ya uhaba wa mafuta unaoshuhudiwa nchini wakati huu.

Kaimu Waziri wa Petroli na Madini Monica Juma sasa atahitajika kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Kawi kutoa maelezo kuhusu namna pesa za hazina hiyo zimekuwa zikitolewa kwa kampuni za mafuta kila mwezi, kuanzia Septemba 2021 hadi sasa.

Wizara hiyo pia itaeleza kiasi cha pesa ambazo hutumwa kwa kampuni kubwakubwa za mafuta na zile kampuni ndogondogo ili kufidia hasara zinazopata kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

Katika ombi hilo ambalo liliwasilishwa na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, waziri Juma pia atahitajika kutoa orodha ya kampuni zilizosajiliwa kuuza mafuta nchini na wafanyabiashara wengine wadogo na vituo vinavyomilikiwa na kampuni hizo.

“Na muhimu zaidi waziri atahitajika kueleza mikakati ya kudumu ambayo wizara yake imeweka kuzuia uhaba wa mafuta katika siku zijazo,” Bw Duale akasema bungeni Jumanne alasiri.

Serikali inaendesha mpango wa kupunguza bei ya mafuta unaogharimu mabilioni ya fedha zinazokusanywa kama ada kutoka kwa watumiaji mafuta.

Pesa hizo huwekwa katika Hazina ya Ustawi wa Sekta ya Petroli. Ada hiyo iliongezwa hadi Sh5.20 kwa lita moja ya mafuta kuanzia Julai 2020 kutoka ada ya zamani ya senti 40.

Pesa za hazina hiyo huwakinga wateja kutokana na ongezeko la bei ya mafuta lakini inawaumiza waendeshaji magari ambao wanalazimia kulipa Sh5.40 zaidi kwa lita moja ya petroli na dizeli.

Serikali inakiri kuwa inadaiwa Sh13 bilioni na kampuni za kuuza mafuta ilhali wafanyabiashara hao wanashikilia kuwa wanadai jumla ya Sh20 bilioni kutoka kwa serikali.

Vuta nikuvute kati ya serikali na kampuni za kuuza mafuta (OMC) imechangia hali ya sasa ambapo kuna uhaba wa mafuta kote nchini. Hii ni baada ya kampuni nyingi za mafuta kuhodhi bidhaa hizo ili ziweze kuuza kwa faida kubwa baadaye.

Mabunge ya Kitaifa na Seneti yameisuta kwa kusababisha shida hiyo kwa kufeli kulipa mabilioni ya fedha za kuzikinga kampuni hizo dhidi ya kupata hasara.

Mnamo Jumanne, mabunge hayo mawili yalijadili suala hilo kwa kina siku moja baada ya Wizara ya Mafuta kutoa Sh8.2 bilioni kwa kampuni za kuuza mafuta. Kiwango hicho cha pesa ni sehemu tu ya jumla ya malipo ambayo kampuni hizo zinadai kutoka kwa serikali.

Mnamo Jumatatu Katibu katika Wizara ya Mafuta Andrew Kamau alisema wizara yake imeanzisha uchunguzi kuhusu chanzo cha uhaba wa mafuta huku akiahidi kwamba kampuni ambazo zitapatikana na hatia ya kuhodhi mafuta zitaadhibiwa.

“Adhabu hiyo itajumuisha faini au kampuni husika kupokonywa leseni,” Bw Kamau akasema.

Katibu huyo wa Wizara aliahidi kuwa hali ya kawaida ya kusambazaji mafuta itarejelea kuanzia Alhamisi, Aprili 7, 2022, baada ya kampuni kubwa za mafuta kuwasilisha bidhaa hiyo kwa vituo vya mafuta kote nchini.

Bw Duale alisema kampuni za mafuta zinakabiliwa na changamoto za kifedha baada ya serikali kufeli kuzilipa pesa chini ya mpango maalum wa upunguzaji bei ya mafuta.

“Hii ndio manaa kampuni hizo zimeamua kuhodhi kiasi kidogo cha mafuta katika hifadhi zao,” Mbunge huyo wa Garissa Mjini akasema.

“Mnamo Machi 14, 2022 Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi Nchini Nchini (EPRA) iliongeza bei ya mafuta aina ya dizeli na petroli kwa kiwango cha Sh5. Lakini licha ya nyongeza hiyo serikali haikutoa pesa za kukinga kampuni za mafuta kutokana na hasara. Hii ilimaanisha kuwa kampuni hizo haziwezi kupata faida kutokana na nyongeza hiyo,” Bw Duale akasema.

Kufuatia nyongeza hiyo bei ya dizeli ilipanda kutoka Sh110 kwa lita moja hadi Sh115 jijini Nairobi na viungani mwake. Nayo bei ya petroli ilipanda kutoka Sh129.7 kwa lita hadi Sh134.7, bei ya juu zaidi kuwahi katika historia ya taifa hili.

Bw Duale aliuliza ni kwa nini serikali iliamua kutenga pesa kupitia bajeti ya ziada kulipa kampuni za mafuta ilhali kuna pesa za Hazina ya Mafuta.

  • Tags

You can share this post!

Msaidizi wa Murkomen pia ahojiwa kuhusu shambulio

Wanafunzi mtaa wa mabanda wakiuka hali ngumu na kufanya...

T L