Kimataifa

Bunge lapitisha sheria kukata idadi ya wabunge, maseneta

October 10th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

ROME, ITALIA

BUNGE la Italia limepitisha sheria ya kutaka idadi ya wabunge na maseneta ipunguzwe kwa asilimia 40 ili kunusuru hela za walipa ushuru.

Sheria hiyo inalenga kupunguza idadi ya wabunge kutoka 630 hadi 400 na maseneta kutoka 315 hadi 200.

Italia ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya maseneta na wabunge ikilinganishwa na mataifa mengineyo ya Muungano wa Ulaya (EU). Uingereza ndiyo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wabunge EU.

Kupunguzwa kwa wabunge na maseneta ni miongoni mwa ahadi zilizotolewa na chama cha Five Star Movement (M5S). Chama cha M5S ndicho kikubwa katika serikali ya muungano unaoongoza nchi hiyo.

Chama hicho kinasema hatua hiyo itasaidia kuokoa mamilioni ya fedha ambazo zimekuwa zikitumika kuwalipa mishahara wabunge hao.

Wakosoaji hata hivyo, wanasema kuwa hatua hiyo itafifisha demokrasia nchini humo.

Sasa raia wa Italia watafanya kura ya maamuzi kuidhinisha sheria hiyo.

Mabadiliko yoyote yanayofanyiwa Katiba ni sharti yapitishwe na raia wote kupitia kura ya maamuzi.

“Tumemaliza! Tumetimiza ahadi tuliyotoa kwa wananchi,” ikasema taarifa ya chama cha M5S kupitia mtandao wa Twitter

Chama hicho kilisema hatua hiyo itasaidia kuokoa Sh113.8 bilioni katika kipindi cha miaka 10.

Mswada wa sheria hiyo uliungwa mkono na karibu vyama vyote bungeni.

“Hii ndiyo siku ambayo tumekuwa tukiingojea kwa miaka mingi. Tumekuwa tukiahidi kupunguza idadi ya wabunge na maseneta lakini ahadi hiyo haijawahi kutimizwa. Lakini kawia ufike, tumefika sasa,” akasema waziri Riccardo Fraccaro.

Kulingana na Shirika la Habari la Italia (AGI), mbunge hupokea mshahara na marupurupu ya Sh26 milioni na seneta hupata Sh28.4 milioni kwa mwaka.

Iwapo itapitishwa na wananchi kupitia kura ya maamuzi, sheria hiyo mpya itaanza kutumika baada ya uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika 2023.

Muungano baina ya chama cha Five Star na chama cha League ulisambaratika Agosti, mwaka huu.

Five Star baadaye kiliungana na chama cha Democratic Party (PD) ambapo viliafikiana kuhakikisha kuwa sheria ya kuwapunguzia mzigo walipa ushuru inapitishwa.

Awali chama cha PD kilikuwa kimepinga mswada huo lakini kikabadili msimamo baada ya kukaribishwa katika serikali ya mseto.

Hiyo ilikuwa mara ya nane kujaribu kupunguza idadi ya wabunge na maseneta tangu 1983.

Lengo kuu la serikali ni kuepuka kuwaongezea raia wa nchi hiyo ushuru.

Chama cha M5S sasa kimeahidi kufanyia mabadiliko sheria za uchaguzi.