Habari Mseto

Bunge latetea wanafunzi wa vyuo vya kiufundi

October 11th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE sasa wanataka Sh2.5 bilioni zilizotengewa Hazina ya Mafunzo ya Kiufundi (TVET) katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 zihamishwe kutoka Wizara ya Elimu na kuwekwa chini ya usimamizi wa bodi ya hazina ya kufadhili mafunzo hayo.

Wanachama wa kamati ya bunge kuhusu uwekezaji (PIC) Jumatano walitoa pendekezo hilo baada baada ya kupata habari kwamba wanafunzi wengi hukosa kunafaika kwa fedha hizo kw sababu ya utaratibu mrefu unaozingatiwa na maafisa wa wizara hiyo kabla ya kuachilia pesa hizo.

“Tunataka sheria ya TVET ifanyiwe marekebisho ili kuhakikisha kuwa Sh2.5 bilioni zilizotengewa TVET zisimamiwe wa bodi ya hazina hiyo. Kwa hivyo, nitawasilisha mswada wa marekebisho ya sheria ili wanafunzi wanaosomea kozi mbalimbali katika vyuo vya kadri wasikose fedha za serikali,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Abdulswamad Nassir.

Bw Nassir alisema bodi hiyo ndio iko katika nafasi bora ya kuwatambua maelfu ya wanafunzi ambao wanafunzi ambayo wanapokea mafunzo katika vyuo vya TVET kote nchini kwa urahisi kuliko wizara ya Elimu.

“Pesa hizo zinafaa kuwanufaisha vijana ambao wanataka kusoma lakini hawana karo wakati huu, lakini hamna uwazi katika wizara ya elimu wakati huu hali inayochangia wanafunzi wengi kuteseka,” akaongeza.

Wanachama wa PIC walisema Sh2.5 bilioni zikigawanya kwa misingi ya Sh30,000 kwa kila mwanafunzi zinaweza kuwafaidi wanafunzi 264 katika kila moja ya maeneo bunge 290 nchini.

Sehemu ya 47 ya Sheria ya TVET inabuni Bodi ya Ufadhili wa TVET yenye wajibu wa kutoa pesa ambazo zitatumiwa kufadhili vyuo vya kutoa mafunzo ya kiufundi kote nchini.