Bungoma imegeuka mbingu yenye mungu, manabii na Yesu

Bungoma imegeuka mbingu yenye mungu, manabii na Yesu

LEONARD ONYANGO Na JESSE CHENGE

ELIJAH MASINDE

NABII wa kwanza kutokea Bungoma alikuwa Elijah Masinde wa Nameme anayeaminika kuzaliwa kati ya 1910 na 1912 katika eneo la Kimilili.

Alichezea timu ya taifa ya Kenya katika Kombe la Gossage dhidi ya Uganda mnamo 1930.

Usiku mmoja Aprili 1943, Masinde alidai kuwa Mungu alimjia alipokuwa usingizini akamwambia: “Mimi ni Wele wa Musambwa. Ninasema kutoka Sayoni kwenye mlima mtakatifu wa Elgon. Nimekuita wewe Masinde uwe kiongozi wa Dini ya Musambwa. Uwaambie Wabukusu wote kumwamini roho wa Musambwa. Watakuwa na chakula tele.”

Masinde alianza kuhubiria watu wa jamii ya Wabukusu kuhusu maneno aliyoambiwa na Mungu. Alipowaambia wasilipe kodi na kuchoma vitambulisho vyao, alitupwa jela na serikali ya Wakoloni.

Mjane wa Elijah Masinde, Bi Gladys Nanjala Masinde akiwa Maeni, Kaunti ya Bungoma. PICHA | MAKTABA

Alipotoka jela, alijenga jumuiya ya ‘Dini ya Musambwa’ na kuwa na wafuasi wengi miongoni mwa Waluhya.

Serikali ya Wakoloni ilishindwa kumwelewa Masinde na kuamua kumchukulia kama mwendawazimu na hivyo basi kumweka katika hospitali ya wagonjwa wa akili ya Mathari, Nairobi kwa miaka miwili.

Mnamo 1948, Masinde alishtakiwa kwa kosa la uhaini na kupelekwa uhamishoni katika kisiwa cha Lamu ambako alikaa hadi 1961.

Dini ya Musambwa ilisajiliwa rasmi mnamo 1964 baada ya Kenya kuwa huru. Lakini baadaye, serikali ya Jomo Kenyatta ilimfunga kwa miaka 15 kwa madai ya kuchochea chuki za kidini. Aliachiliwa na serikali ya Daniel arap Moi.

Mnamo 1978, Moi pia alimkamata kufuatia makabiliano yake na polisi wa trafiki eneo la Webuye na Kitale. Kabla ya kifo chake, Masinde alisema kuwa jamaa yake mmoja alimroga.

JEHOVA WANYONYI

Inaaminika kuwa Michael Mwaboyi, maarufu kwa jina la Jehova Wanyonyi alizaliwa 1924.

Alidai kuwa yeye alikuwa mungu na kwamba Yesu ni mwanawe. Jehova Wanyonyi alikuwa na wake 70 na alidai kuwa na nguvu za kuponya virusi vya HIV. Alitaka serikali imlipe Sh3 bilioni ili afagie virusi vya HIV kutoka nchini Kenya.

Ingawa wafuasi wake wapatao 1,000 wanaamini yuko hai, Wanyonyi alifariki dunia mnamo 2015 akiwa na umri wa miaka 91.

NABII YOHANA (V)

Katika kijiji cha Nandolia, eneobunge la Kanduyi, Geofrey Nakalira Wanyama alichipuka na kuanza kujiita Nabii Yohana (V).

Nabii Yohana (V) . PICHA | MAKTABA

Yohana wa Tano aliye na umri wa miaka 83, ameandika biblia yake na ana zaidi ya wake 30 na wanafunzi 12. Biblia yake ina vitabu 93 badala ya 66 vilivyo katika Biblia Takatifu ya Wakristo.

Anadai kuwa amekuja na amri 12 badala ya amri 10 ambazo Mungu alimpa Musa Mlimani Sinai.

  • Tags

You can share this post!

Ana kijichumba cha wafuasi kujitakasa

KINYUA KING’ORI: Vinara wa Azimio wana hoja nzito za...

T L