Michezo

Bungoma njiapanda katika magongo ya Supa Ligi

August 12th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya Bungoma Farmers iliendelea kudorora kwenye kampeni za magongo ya Supa Ligi baada ya kucharazwa magoli 2-1 na Chuo Kikuu cha Kenya College of Accountancy (KCA) uwanjani City Park, Nairobi.

Wachezaji wa timu hizo waliteremka dimbani tayari kupigania alama tatu muhimu huku kila upande ukishambulia kutafuta magoli ya mapema. Philip Kitui aliiweka KCA kifua mbele kabla ya Samuel Ongachi kusawazishia Bungoma Farmers dakika kumi baadaye.

Hata hivyo Kelvin Oduor aliisaidia KCA kuvuana ufanisi huo alipoitingia bao la tatu dakika tatu kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa.

Kufuatia matokeo hayo, wasomi wa KCA wanaendelea kujiongezea matumaini ya kufanya vizuri na kupandisha ngazi kuerejea kushiriki mechi za ngarambe ya Ligi Kuu muhula ujao.

Kwenye mfululizo wa mechi hizo, TUK iliandikisha pointi moja baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Wazalendo Masters nayo timu ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) iliagana sare tasa na Mombasa Sports Club (MSC). TUK ilifungiwa na Evans Odhiambo huku bao la MSC likifumwa kimiani na Richard Njuki.

Kwenye jedwali ya kipute hicho, wanazuo wa KCA wameshikilia mbili bora kwa kuvuna alam 21, moja mbele ya MSC baada ya kila moja kucheza mechi 11. Nao wanaume wa kikosi cha Parkroad Badgers wangali kileleni mwa jedwali kwa kufikisha alama 33.